• HABARI MPYA

  Monday, January 22, 2018

  YANGA KUMKOSA BUSWITA MECHI NA AZAM, ILA CHIRWA NA YONDAN WATAKUWEPO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC itamkosa kiungo wake mshambuliaji tegemeo kwa sasa, Pius Charles Buswita katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Jumamosi ijayo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Hiyo ni baada ya mchezaji huyo aliye katika msimu wake wa kwanza Jangwani tangu asajiliwe kutoka Mbao FC ya Mwanza kuonyeshwa kadi ya njano ya tatu jana katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Yanga iliichapa 1-0 Ruvu jana, bao pekee la Buswita dakika ya 45 na ushei kwa kichwa akimalizia krosi ya Ibrahim Ajib Migomba, kabla ya kuonyeshwa kadi ya njano dakika ya 69 kwa kumchezea rafu beki wa wapinzani, Rajab Zahir.
  Lakini habari njema kwa Yanga ni kwamba, mshambuliaji wake tegemeo la mabao kwa sasa, Obrey Chirwa anarejea baada ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa mechi tatu kwa kumpiga mchezaji wa Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Novemba 25, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex.
  Pamoja na kufungiwa mechi tatu, Chirwa pia alitozwa faini ya Sh. 500,000 kwa kosa hilo kwenye mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1, maamuzi yaliyofikiwa kwenye kikao cha Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Januari 14, mwaka huu 2018 mjini Dar es Salaam.
  Habari nyingine njema kwa wana Yanga ni kurejea kwa beki wa kati mkongwe, Kevin Yondan aliyekosekana kwenye mechi na Ruvu Shooting kutokana na adhabu ya kadi tatu za njano pia.
  Ligi Kuu inaendelea leo kwa mechi mbili za kukamilisha mzunguko wa 14, mjini Bukoba mkoani Kagera, wenyeji Kagera Sugar watawakaribisha Simba SC Uwanja wa Kaitaba na Uwanja wa Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma, wenyeji Maji Maji watawakaribisha Singida United.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KUMKOSA BUSWITA MECHI NA AZAM, ILA CHIRWA NA YONDAN WATAKUWEPO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top