• HABARI MPYA

  Sunday, January 21, 2018

  NANI KAWATAFUTIA SIMBA HUYU PIERRE LECHANTRE?

  KITENDAWILI cha nani atakuwa kocha mpya Mkuu wa Simba SC kiliteguliwa Ijumaa baada ya kaimu Rais wa klabu, Salim Abdallah ‘Try Again’ kumtambulisha Mfaransa, Pierre Lechantre katika hafla maalum iliyofanyika ukumbi wa Kivukoni 4, hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam.
  Abdallah aliwasainisha mikataba Lechantre pamoja na Msaidizi wake, kocha wa mazoezi ya viungo, Mtunisia Mohammed Aymen Hbibi na akasema wataalamu hao wanaingia Simba SC kwa ajili ya programu maalumu ya kuinoa timu ya wakubwa na wadogo.
  Lechantre ambaye ataanza kazi timu itakaporejea kutoka Bukoba ambako kesho itamenyana na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Kaitaba, amesema anaomba apewe angalau miezi minne ili wana Simba waanze kufurahia kazi yake. 
  Pierre Lechantre aliyezaliwa Aprili 2, mwaka 1950 mjini Lille, Nord, Ufaransa ni kocha aliyeipa Cameroon ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2000 na kabla ya kuanza kufundisha alikuwa mchezani pia.
  Aprili 27 mwaka 2012, Lechantre alitambulishwa kuwa kocha Mkuu wa Senegal, lakini akashindwa kufikia makubaliano ya mwisho na Shirikisho la Soka la nchi hiyo.
  Akiwa mchezaji katika nafasi ya ushambuliaji, Lechantre amechezea klabu za Paris FC (1986–1989), Red Star 93 (1983–1986), Stade de Reims (1981–1983), Olympique de Marseille (1980–81), RC Lens (1979–80), Stade Lavallois (1976–1979), AS Monaco (1975–76), FC Sochaux (1970–1975) na Lille OSC (1964–1970).
  Na akiwa kocha amefundisha timu za taifa za Kongo (2016), Cameroon (1999-2001), klabu za Al-Ittihad Tripoli ya Libya kuanzia 2014 hadi 2015, Al Arabi ya Qatar kuanzia Machi hadi September 2013, CS Sfaxien ya Tunisia kuanzia Juni hadi Desemba 2010, Club Africain ya Tunisia kuanzia Juni 10 mwaka 2009 hadi Aprili 2010 na Al Rayyan ya Qatar.
  Amefundisha pia timu ya taifa ya Mali kuanzia Machi hadi Oktoba 2005, Al-Siliya Sports Club ya Qatar kuanzia Novemba 2003, Al-Ahli ya Jeddah kuanzia Agosti hadi Oktoba mwaka 2003, Qatar kuanzia Juni 2002, Le Perreux (1992–1995) na Paris FC (1987–1992).
  Amewahi pia kuwa Mshauri wa Ufundi wa Val de Marne kuanzia Julai 7 mwaka 1995 hadi Januari 1999.
  Kwa wasifu huu, wazi Simba SC kwa mara nyingine imepata kocha mzuri kitaaluma, aliyebobea na mwenye rekodi ya kushinda mataji.
  Naye amekuwa na bahati ameikuta timu ipo vizuri pia, kwani Alhamisi aliishuhudia ikishinda 4-0 dhidi ya timu ngumu, Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Hiyo ni kazi nzuri ya mwalimu wa muda, Mrundi Masoud Juma ambaye sasa atarejea kuwa kocha Msaidizi chini ya Lechantre.
  Kwa sababu Juma anazungumza Kiingereza, Kiswahili na Kifaransa atakuwa akisaidia pia kufikisha ujumbe kwa wachezaji kutoka kwa makocha wanaozungumza Kifaransa, Lechantre na Mohammed Aymen Hbibi.
  Ni matarajio kabisa mseto wa watatu hawa, Lechantre, Juma na Aymen Hbibi pamoja na kocha wa makipa, mzawa Muharami Mohammed ‘Shilton’ utakwenda kufanya kazi nzuri, vizuri na kwa maelewano na ufanisi wa hali ya juu Simba SC.
  Inawezekana ujio wa kocha mpya bila shaka ukaendana na mabadiliko ya falsafa na mfumo wa timu, lakini ni matumaini pia hayo yatafanyika kwa tahadhari ili yasije yakaivuruga timu katikati ya kampeni.
  Kitu kimoja tu ambacho ni shaka kubwa, ni kwamba watu hawana imani na Simba SC kama itadumu na mwalimu huyo kutokana na desturi yao ya kufukuza fukuza walimu bila hata sababu za msingi. 
  Na hiyo ni kwa sababu viongozi wa klabu zetu siku hizi wamejiruhusu kufanya kazi kwa shinikizo la mashabiki na si kuzingatia weledi tena.
  Wakati wote viongozi wa klabu wamekuwa wakitaka kujikosha mbele ya wapenzi, wanachama na mashabiki kwa gharama yoyote, ikibidi kuwatoa kafara wachezaji na makocha na hiyo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo yetu kisoka.  
  Naamini mchakato wa kumapata mrithi wa Mcameroon, Joseph Marius Omog ulikuwa makini na ndiyo maana mwisho wa siku amepatikana Lechantre, kocha bora kwa kutazama tu rekodi yake hata kaba hajaanza kazi.  
  Huyo ni kocha ambaye ametafutwa na viongozi wenyewe wa Simba SC chini ya Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ iwe kwa wao wenyewe kumtafuta moja kwa moja au kupitia kwa wakala, lakini mwisho wa siku waliridhika naye na hatimaye wamempa mkataba.
  Lazima Simba wanajua wametoka wapi na wanakwenda wapi, kwamba kuachana na Omog na kumkabidhi timu Lechatre ni hatua ambayo waliitaka wenyewe na wanajua wanachotarajia.
  Hivyo basi ni matarajio yetu kwamba ndoa iliyofungwa Ijumaa itadumu baina ya pande hizo mbili, kwa sababu Lechantre ni kocha waliyemtafuta wenyewe Simba. Kila la heri.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NANI KAWATAFUTIA SIMBA HUYU PIERRE LECHANTRE? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top