• HABARI MPYA

    Wednesday, January 10, 2018

    MAGWIJI WATATU WAPEWA UBALOZI WA CHAN 2018

    MAGWIJI watatu, Nourredine Naybet wa Morocco, Robert Kidiaba wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Adel Chedli wa Tunisia wameteuliwa kuwa Mabalozi wa michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) nchini Morocco 2018.
    Watatu hao wamepewa hadhi hiyo kutokana na mchango wao mkubwa kwenye michuano hiyo na kwenye soka ya bara la Afrika kwa ujumla kutokana na michuano mbalimbali waliyocheza.
    Naybet ni kipenzi cha mashabiki nchini mwake, Morocco ambaye alizaliwa mjini Casablanca, ambako aling’ara kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1992 kabla ya kutimia Ulaya na katika miaka yake 16 ya kuwa uwanjani, aliwachezea Simba wa Atlasi katika mechi 115.
    Robert Kidiaba wa DRC ameteuliwa kuwa Balozi wa CHAN ya mwaka huu nchini Morocco 

    Mshindi wa CHAN ya kwanza mwaka 2009 akiwa na DRC, Kidiaba amejipatia mafanikio makubwa akiwa na vigogo wa Lubumbashi, TP Mazembe, ambako amefanikiwa kushinda mataji yote ya nyumbani na ya bara la Afrika. Ni umaarufu kwa mtindo wake wa kushangilia bao kwa kuruka ruka kwa kujiburuza makalio.
    Februari 25 mwaka  2011 mjini Omdurman, Sudan, Chedli aliweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza na pekee kushinda mataji yote, Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na CHAN. Mchezaji wa kikosi cha Tunisia kilichoshinda taji la AFCON mwaka 2004, akashinda na CHAN akiwa ana umri wa miakia 35 Tunisia ikiifunga Angola 3-0 kwenye fainali mwaka 2011.
    Michuano ya CHAN inatarajiwa kuanza Januari 13 hadi Februari 4 mwaka huu mjini Casablanca, Morocco.
    Kundi A linaundwa na timu za Morocco, Mauritania, Guinea na Sudan, Kundi B kuna Namibia, Uganda, Zambia na Ivory Coast, Kundi C kuna Libya, Nigeria, Rwanda na Equatorial Guinea wakati Kundi D linaundwa na Kongo, Angola, Cameroon na Burkina Faso.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAGWIJI WATATU WAPEWA UBALOZI WA CHAN 2018 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top