• HABARI MPYA

  Wednesday, January 17, 2018

  BENCHI LA UFUNDI LAENDELEA KUIGHARIMU YANGA, YASHINDWA KUIFUNGA NA MWADUI LEO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KWA mara nyingine makosa ya benchi la Ufundi la Yanga kupanga wachezaji wasio fiti na kuwaacha benchi vijana wadogo walio fiti yameigharimu timu kulazimishwa sare ya 0-0 na Mwadui FC ya Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jioni ya leo.
  Yanga ilimuanzisha mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe ambaye ametoka kuugua Malaria huku ikiwaacha benchi chipukizi kama Yohanna Oscar Nkomola na Said Mussa ‘Ronaldo’ walio fiti matokeo yake safu yake ya ushambuliaji ikawa butu leo.
  Tambwe alionekana kabisa hayuko fiti, kwa sababu alicheza chini ya kiwango na akaikosesha timu nafasi kadhaa za kufunga.
  Beki wa Mwadui FC, Iddi Mobby akiupitia mpira miguuni mwa mshambuliaji Amissi Tambwe wa Yanga leo
  Chipukizi Said Mussa 'Ronaldo' akibinuka kibaiskeli kupiga mpira langoni mwa Mwadui 
  Beki Hassan Kessy akijaribu bila mafanikio kuunganisha krosi, mpira ukifika mikononi mwa kipa
  Benchi la Ufundi la Yanga likiwa kazini leo Uwanja wa Uhuru
  Kiungo Emmanuel Martin akimiliki mpira mbele ya beki wa Mwadui

  Safu ya ushambuliaji ya Yanga ilichangamka na kuanza kulitia misukosuko lango la Mwadui baada ya kuingia chipukizi Said Ronaldo na Nkomola waliokwenda kucheza pamoja na kaka yao Ibrahim Ajib pale mbele. Bahati mbaya, Ajib naye leo hakuwa katika ubora wake.
  Yanga ilifanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Mwadui FC, lakini ikashindwa kupata bao kutokana na wageni kuamua kucheza kwa kujihami mwishoni mwa kipindi cha pili.
  Kipindi cha kwanza Mwadui ikiongozwa na mshambuliaji wake mkongwe, Paul Nonga ilitawala mchezo na kipindi cha pili Yanga walizinduka na kuuteka mchezo.
  Makosa kama hayo makocha wa Yanga waliyafanya wiki iliyopita katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya URA wakimpanga Mzambia, Obrey Chirwa ambaye hakuwa fiti na kuwaacha vijana wadogo benchi na kuipoza timu kutolewa kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
  Kama Tambwe leo, siku hiyo Chirwa hakuwa fiti kwa sababu ndiyo alikuwa amejiunga na timu akitokea kwao, Zambia alipokwenda ili kushinikiza alipwe fedha zake za usajili. Lakini pamoja na kwamba alifika Zanzibar siku ya mechi akapangwa na akacheza chini ya kiwango kabisa – na mbaya zaidi akaenda kukosa hadi penalti.
  Leo Yanga imeendelea kuongozwa na makocha Wasaidizi, Mzambia Noel Mwandila na wazalendo Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali, na kocha Mkuu, Mzambia, George Lwandamila alikuwa jukwaani kwa madai hana kibali cha kufanya kazi nchini. 
  Lwandamina alikuwa kwao, Zambia tangu Desemba mwaka jana, kwanza kuhudhuria hafla ya mwanaye wa kike kuhitimu masomo ya chuo, na akiwa huko ukatokea msiba wa mwanawe wa kiume uliomfanya akae kwa muda mrefu kabla ya kurejea nchini wiki iliyopita.
  Matokeo ya 0-0 yanazidi kuitoa Yanga kwenye mbio za ubingwa, ikifikisha pointi 22 baada ya kucheza mechi 13, sasa wakizidiwa pointi nne na vinara Simba na Azam FC ambao pia wana mechi moja moja mikononi.
  Simba watateremka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho kumenyana na Singida United wakati, Azam FC watakuwa Uwanja wa Maji Maji mjini Songea kumenyana na wenyeji, Maji Manji katika mechi za kukamilisha mzunguko wa 13 wa Ligi Kuu.  
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan, Said Juma ‘Makapu’/Raphael Daudi dk68, Juma Mahadhi/Yohanna Nkomola dk77, Pius Buswita, Amissi Tambwe/Said Mussa dk50, Ibrahim Ajib na Emmanuel Martin.
  Mwadui FC; Arnold Massawe, Jackson Salvatory, David Luhende, Joram Mgeveke, Iddy Mobby, Jean Claude John/Morris Malako dk55/Athumani Rajab dk80, Awesu Ally, Awadhi Juma, Paul Nonga, Evarist Mujwahuki na  Abdallah Seseme. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BENCHI LA UFUNDI LAENDELEA KUIGHARIMU YANGA, YASHINDWA KUIFUNGA NA MWADUI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top