• HABARI MPYA

  Sunday, December 11, 2016

  WANACHAMA SIMBA WAPITISHA MABADILIKO YA KATIBA KWA KISHINDO

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  HATIMAYE wanachama wa Simba leo wamepitisha kipengele cha uendeshwaji wa klabu kwa muundo wa hisa katika mkutano maalum wa mabadiliko ya Katiba uliofanyika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.
  Katika mkutano huo ulioongozwa na Rais wa klabu, Evans Elieza Aveva na kuhudhuriwa na wanachama 642 kati ya zaidi 5,000 wa klabu hiyo – mabadiliko ya Katiba yalipita kwa kishindo.
  Wanachama wengi waliunga mkono na watulivu muda wote wa mkutano kufuatilia kwa makini kipengele kimoja hadi kingine kati ya vilivyojadiliwa.
  Kipengele hicho cha uendeshwa wa klabu kwa hisa kitawekwa katika ibara ya 49 ya klabu ya Simba.
  Wanachama wa Simba wakinyoosha mikono kuunga mkono mabadiliko ya Katiba 
  Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka kulia Salim Abdallah, Said Tuliy na Jasmine Costa
  Muongoza mkutano, Wakili Evodius Mtawala akiuliza maoni ya wanachama juu ya Katiba

  Vipengele vingine vyote vidogo vilivyomo ndani ya Ibara hiyo vilipitishwa pia kama cha 49 (i) kinachosomeka; Uamuzi wowote wa kubadilisha mfumo, kuvunja au kufutwa kwa Simba unahitaji theluthi ya 2/3 za wanachama wote wa Simba waliopatikana katika mkutano mkuu uliopitishwa maalum kwa madhumuni hayo.
  Kipengele cha 49 (ii) kinasomeka; Hakutakuwa na mabadiliko na kipengele cha 49(iii) kinasomeka; Kuwepo na sababu za kubadilisha mfumo, kuvunja au kufutwa kwa Simba kama vile kuwa na madeni makubwa yasiyolipika, kupoteza hadhi ya kutoaminika na kukopesheka au kuendana na matakwa ya mfumo wa nyakati za biashara.
  Katika ibara 49 (a) kipengele kilichopitishwa kinasema mkutano wa wanachama unaweza kuitishwa kwa mujibu wa Ibara ya 22 na kufanya mabadiliko ya mfumo wa umiliki au uendeshwaji wa Simba.
  Kwa upande wa kipengele (b) chenyewe kinasema mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji au umiliki wa Simba hayataathiri hadhi ya wanachama wote halali wa Simba isipokuwa hadhi hiyo itabadilika kuendana na mfumo stahiki wa mabadiliko yaliyofanyika.
  Uwiano wa thamani ya umiliki wa kila mwanachama katika mfumo mpya utajadiliwa na Kamati ya Utendaji kutokana na thamani ya klabu na uwekezaji.
  Kipengele (c) cha ibara hiyo kinaeleza kuwa mfumo mpya wa mabadiliko ya uendeshaji au umiliki wa Simba utarithi haki na mali zote pamoja na madeni na wajibu wowote uliokuwa chini ya Simba kabla ya mabadiliko hayo.
  Kipengele (d) na cha mwisho cha Ibara hiyo kinasema mabadiliko ya mfumo wa umiliki au uendeshaji wa Simba yatabainisha kuacha kutumika kwa katiba hii na mkutano mkuu chini ya mfumo mpya utapitisha katiba mpya chini ya utaratibu wa haki na kura za mfumo huo mpya.
  Baada ya wanachama kupitisha kipengele hicho, Rais Aveva aliwataka kuwa watulivu wakati huu ambao mabadiliko hayo yatapelekwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na mwisho kwa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo ili yapitishwe na kuwa Katiba kamili.
  Mkutano huo unafuatia mwanachama wa Simba na mfanyabiasha maarufu nchini Mohamed ‘Mo’ Dewji kutoa ofa ya kununua asilimia 51 ya hisa za klabu hiyo kwa Sh. Bilioni 20.
  Hata hivyo, Baraza la Wadhamini la klabu, chini ya Mwenyekiti wake, Hamisi Kilomoni lilipinga Mkutano huo likitaka kwanza wanachama wahakikiwe na Baraza la Michezo. Hakukuwa na kiongozi wa BMT wala Serikali kwa ujumla kwenye mkuatano huo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WANACHAMA SIMBA WAPITISHA MABADILIKO YA KATIBA KWA KISHINDO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top