• HABARI MPYA

    Sunday, December 18, 2016

    SIMBA NA YANGA ‘ZINAVYOJITAHIDI’ KUUA VIPAJI VYA CHIPUKIZI NCHINI

    MECHI za mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mshambuliaji Ibrahim Hajib alianza kupoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.
    Hajib alikuwa anaanzishiwa benchi, huku kocha Mcameroon Joseph Marius Omog akiwaanzisha pamoja wageni, Mrundi Laudit Mavugo na Frederick Blagnon kutoka Ivory Coast.
    Hajib anauanza mzunguko wa pili akiwa na jukumu la kupigania nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza cha Simba, baada ya kuipoteza mwishoni mwa mzunguko wa kwanza.
    Upande wa Yanga, mshambuliaji Malimi Busungu alisusa tangu Oktoba 1, mwaka huu na kuamua kukaa nyumbani kutokana na kutopewa nafasi kikosi cha kwanza.
    Busungu akaamua kurudi baada ya mabadiliko ya benchi la Ufundi, kocha Mholanzi Hans van der Pluijm akimpisha Mzambia George Lwandamina.
    Awali ya hapo, mshambuliaji mwingine Paul Nonga alishinikiza kuondoka Yanga baada ya nusu msimu tu tangu asajiliwe kutokana na kutokuwa na nafasi kwenye kikosi cha kwanza, akarejea Mwadui FC.
    Mshambuliaji mwingine Matheo Anthony ameendelea kuwashuhudia wageni, Mzimbabwe Donald Ngoma, Mzambia Obrey Chirwa na Mrundi Amissi Tambwe wakicheza Yanga, huku yeye akiwa benchi muda mwingi.
    Na kwa ujumla Simba na Yanga zimejitahidi wakati wote kukamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni na ambao wote wanakuwa muhimu kwenye timu.
    Pale Azam FC  napo baada ya muda mrefu wa John Bocco kuwa na nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza, sasa kuna hatari ya mambo kuanza kumuendea kombo baada ya usajili wa washambuliaji kutoka Ghana dirisha dogo.
    Azam imesajili washambuliaji watatu wa Ghana, Samuel Afful, Daniel Atta Agyei na Yahaya Mohammed maana yake sasa  Nahodha Bocco atakuwa na mtihani mkubwa wa kupigania nafasi yake.
    Kwa muda sasa Bocco amekuwa mshambuliaji tegemeo timu ya taifa kati ya wachezaji wanaocheza nchini, kwa sababu tu amekuwa akipata nafasi ya kucheza Azam.
    Mapema mwaka huu, Hajib alianza kuchomoza kama mshambuliaji mwingine atakayekuja kuwa tegemeo la timu ya taifa ya Tanzania, kutokana na kupata nafasi ya kucheza Simba hivyo kujikusanyia uzoefu na kukuza kiwango chake.
    Zaidi ya hapo, makocha wa timu za taifa wamelazimika kumulika timu nyingine nje ya Azam, Simba na Yanga kupata wachezaji wazuri wazawa.
    Na sasa hali imekuwa mbaya zaidi kwamba hadi makipa, viungo nao pia wanasajiliwa kutoka nje – maana yake utafika wakati hadi makipa wa timu ya taifa watatafutwa timu za mikoani.
    Wakati tunakwenda kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, Simba imemsajili mshambuliaji kinda wa Stand United, Pastory Athanas aliyekuwa anainukia vizuri.
    Athanas aling’ara katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu akifunga bao zuri pekee na la ushindi Stand ikiwalaza mabingwa watetezi, Yanga 1-0 mjini Shinyanga.
    Yanga nayo ikamsajili mshambuliaji chipukizi Emmaniel Martin  wa JKU ya Zanzibar baada ya kumuona katika mchezo mmoja tu.
    Martin aliifungia JKU mabao yote ikiifunga Yanga 2-0 katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Uhuru Jumamosi ya wiki iliyopita na siku iliyofuata akasajiliwa Jangwani.
    Martin anakwenda Yanga ambako wachezaji wenye uzoefu zaidi yake Matheo Anthony na Busungu hawana nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
    Athanas anakwenda Simba ambako Hajib mweye ujuzi na uzoefu zaidi yake anakabiliwa na changamoto ya kupigana kurudi kwenye kikosi cha kwanza.
    Simba imemrudisha Azam FC mshambuliaji Ame Ali iliyemchukua kwa mkopo mwanzoni mwa msimu. Ame aliondoka Mtibwa Sugar msimu uliopita akiwa mshambuliaji tegemeo kwenda Azam ambako hakufanikiwa kupata nafasi hadi kushusha kiwango.
    Simba wakikumbuka ubora wake alipokuwa Mtibwa, wakaamua kumuomba kwa mkopo. Ame hakupata nafasi Simba, lakini katika mechi chache alizopangwa alicheza vizuri.
    Ame aliondoka Mtibwa kwenda Azam akiwa amekwishaanza kuitwa timu ya taifa. Busungu pia aliondoka Mgambo JKT kwenda Yanga akiwa amekwishaanza kuitwa timu ya taifa na sasa wote wamepoteza nafasi kwa sababu uwezo umeshuka kutokana na kukosa nafasi ya kucheza.
    Wachezaji wazuri hawakai kweye timu zao zinazowapa nafasi ya kucheza kwa sababu ya ushawishi wa Azam, Simba na Yanga zinazowafuata na ofa nzuri baada ya kung’ara kidogo.
    Lakini haziwachukui kuwaendeleza, bali kwenda kuuwa viwango vyao na baadaye kuwatupa. Na wachezaji hawawezi kuacha fedha nzuri za timu hizo wanapofuatwa, kwa sababu wanacheza mpira kuzitafuta hizo hizo fedha na si kujifurahisha. 
    Kilichobaki ni kutazama kama Athanas ataweza kazi iliyomshinda Ame Ali, au Martin atauweza mfupa uliomsinda Paul Nonga. 
    Lakini hivyo ndivyo namna ambavyo Simba na Yanga zinavyojitahidi kuua vipaji vya wachezaji chipukizi nchini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA ‘ZINAVYOJITAHIDI’ KUUA VIPAJI VYA CHIPUKIZI NCHINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top