• HABARI MPYA

    Wednesday, December 07, 2016

    POWER DYNAMOS YA ZAMBIA KUIPIMA SIMBA ‘MAULID DAY’ DAR

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC inatarajiwa kushuka dimbani Desemba 12, mwaka huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kumenyana na Power Dynamos ya Zambia.
    Mchezo huo utakaochezwa siku ya sherehe za Maulid kuazimisha kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W.) ni maalum kwa kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog kumjaribu kipa mpya, Daniel Agyei kutoka Medeama SC ya Ghana.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam kwamba kikosi cha timu hiyo kinaendelea na mazoezi mjini Morogoro.
    Manara amesema kwamba kikosi kitawasili Dar es Salaam asubuhi ya kuamkia mchezo huo, Jumatatu – na baada ya hapo kitaendelea na maandalizi ya mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tnzania Bara mzunguko wa pili dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara.   
    Wachezaji wa Simba waliopo kambini Morogoro ni makipa; Vincent Angban, Peter Manyika, Daniel Agyei, na Dennis Richard, mabeki; Hamad Juma, Janvier Bokungu, Abdi Banda, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Emmanuel Semwanza, Malika Ndeule, Novaty Lufunga na Method Mwanjali.
    Viungo ni Awadh Juma, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, Mussa Ndusha, Muzamil Yassin, Jamal Mnyate, Shizza Kichuya na washambuliaji Frederick Blagnon, Laudit Mavugo, Ame Ally na Ibrahim Hajib na Hajji Ugando.
    Mchezaji pekee anayekosekana Simba kwa sasa ni beki Mganda, Juuko Murshid, ambaye ana ruhusa maalum, yupo na timu yake ya taifa inayojiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Gabon mwezi ujao.
    Simba ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika nafasi ya kwanza kwa pointi zake 35, mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga. 
    Wakati huo huo: Baraza la Wazee la Simba SC limewahimiza wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa kubadilisha Katiba Jumapili ya Desemba 11, mwaka huu ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
    Hata hivyo, mkutano huo umepingwa na Baraza la Wadhamini la klabu, lililoelekeza taratibu kadhaa zifuatwe kwanza, ikiwemo uhakiki wa wanachama chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: POWER DYNAMOS YA ZAMBIA KUIPIMA SIMBA ‘MAULID DAY’ DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top