• HABARI MPYA

  Tuesday, May 16, 2023

  NABI: MATOKEO YA MECHI YA KWANZA NA GALLANTS TUMETUPA HUKO


  KOCHA wa Yanga SC, Mtunisia Nasredeen Mohamed Nabi amesema kwamba wataingia kwenye mchezo wa kesho wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Marumo Gallants kusaka ushindi mwingine.
  Akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari leo kuelekea mchezo wa kesho utakaoanza Saa 1:00 usiku Uwanja wa Royal Bafokeng mjini, Phokeng Jijini Rustenburg amesema wameyaweka kando matokeo ya ushindi wa 2-0 kwenye mchezo wa kwanza nyumbani, Dar es Salaam.
  "Tumesahau kuhusu faida ya ushindi wa 2-0 tulioupata kwenye uwanja wa nyumbani. Huu ni mchezo mwingine na tuko na mpango mwingine wa dakika 90 za hapa,” amesema Nabi na kuongeza.
  "Ni jambo zuri Marumo wamepanga mechi isiwe na kiingilio. Sisi kama Yanga tunapenda kucheza mbele ya mashabiki wengi kuliko uwanja kukosa mashabiki. 
  “Nina wachezaji wenye uzoefu wa kutosha wa kucheza mechi za namna hii,”.
  Kwa upande wake mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda amesema wao kama wachezaji wako tayari kwa mechi hiyo ya kihistoria.
  "Maandalizi ni mazuri sana kwa upande wetu wachezaji na tunajua tumekuja kwenye mchezo mkubwa. Tuko tayari kupambana na kurudi nyumbani tukiwa washindi,” amesema Kennedy Musonda.
  Pamoja na taarifa kwamba wachezaji wa Marumo Gallants wamegoma kufanya mazoezi kwa sababu wanadai posho, lakini Kocha Msaidizi Raymond Mdaka  aliambatana na Nahodha Washington Arubi kwenye mkutano na Waandishi wa Habari na kusema wapo tayari kwa mchezo wa kesho ili wapindue matokeo na kwenda Fainali.
  Mchezo mwingne wa marudiano wa Nusu Fainali utafuatia Saa 4:00 usiku kesho Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers kati ya wenyeji, USM Alger na ASEC Mimosas ambazo mechi ya kwanza zilitoka sare ya 0-0 Uwanja wa Bouaké, Ivory Coast.
  Ikumbukwe Fainali za Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu zitachezwa Mei 28 na Juni 3.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NABI: MATOKEO YA MECHI YA KWANZA NA GALLANTS TUMETUPA HUKO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top