• HABARI MPYA

  Thursday, May 18, 2023

  RAIS DK SAMIA KUWAPA NDEGE YANGA KWENDA ALGERIA NA MOTISHA JUU


  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwapa ndege Yanga kwenda kwenye mchezo wa marudiano wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger nchini Algeria mapema mwezi ujao.
  Mheshimiwa Rais Dk. Samia ametoa ahadi hiyo mchana wa leo akizungumza kwenye hafla ya miaka 10 ya Azam Media Limited, Tabata Jijini Dar es Salaam.
  Pamoja na hilo, Rais Samia ameahidi kutoa Sh. Milioni 20 kwa kila bao ambalo Yanga watafunga kwenye michezo miwili ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
  “Sasa nitumie jukwaa hili hiki kuipongeza timu yetu ya Yanga, wameingia na timu yetu ya Simba, wamecheza kwenye hayo mashindano vizuri. Na niliwapa msukumo kidogo, wamefanya vizuri lakini kwa bahati moja imeishia katikati, Yanga imeendelea, nawapongeza sana,”.
  “Sasa Yanga inakwenda kwenye Fainali, si ndiyo? Sasa niseme yafuatayo; nilianza na mechi hizi kwa Sh. Milioni 5 kwa kila goli la ushindi, waliposogea nikasema sasa Milioni 10 kwa kila goli la ushindi, tunapokwenda kwenye Fainali ni Milioni 20 timu ikitoka na ushindi,”:
  “Milioni 20 hii haitakwenda kafunga mbili kafungwa moja. Hapana, yawe magoli yote yameipa timu hiyo ushindi, kila goli Milioni 20.
  Lakini zaidi ya hapo, Serikali itatoa ndege kuwapeleka katika mchezo wa Fainali. Sasa ndege hiyo itabeba wachezaji, itabeba washabiki, na ninaomba sana, wale viongozi wa TFF na mchezo huu kuwapa moyo kama Serikali tunavyofanya,”
  Yanga SC jana ilifanikiwa kwenda Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Marumo Gallants Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng NW Jijini Rustenburg nchini Afrika Kusini.
  Ilikuwa siku nzuri ofisini kwa mshambuliaji wa Kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Fiston Kalala Mayele aliyefunga bao la Kwanza dakika ya 45, kabla ya kumsetia Mzambia, Kennedy Musonda kufunga la pili dakika ya 62.
  Marumo Gallants walipata bao lao pekee kupitia kwa mshambuliaji wao, Ranga Piniel Chivaviro dakika ya 90 na ushei, hivyo kuendelea kufungana na Mayele kwneye chati ya ufungaji kila mmoja akiwa na mabao saba.
  Yanga wanakwenda Fainali kwa ushindi wa jumla wa 4-1 kufuatia kuwafunga Marumo Gallants 2-0 kwenye mchezo wa Kwanza Jumatano iliyopita Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Yanga itaanzia nyumbani katika Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger Mei 28 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Algeria kwa mchezo wa marudiano Juni 3 Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers.
  USM Alger imeitoa ASEC Mimosas ya Ivory Coast baada ya sare ya 0-0 ugenini na ushindi wa 2-0 nyumbani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS DK SAMIA KUWAPA NDEGE YANGA KWENDA ALGERIA NA MOTISHA JUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top