• HABARI MPYA

  Wednesday, May 24, 2023

  MKUU MPYA WA MKOA DAR ANUNUA TIKETI 1,000 YANGA NA USM ALGER


  MKUU mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamilla amenunua tiketi za Sh. Milioni 5 kwa ajili ya mashabiki kuelekea mchezo wa kwanza wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya wenyeji, Yanga SC dhidi ya USM Alger Jumapili Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Chalamila amemkabidhi Fedha hizo Rais wa Yanga, Hersi Said ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam na akasema atakabidhiwa mwenyewe tiketi hizo 1,000 akazigawe kwa watu wa kipato cha chini wakaishangilia Yanga Jumapili.
  Pamoja na fedha hizo, Chalamila amekabidhi Sh. Milioni 5 nyingine kwa ajili ya kutayarishwa chakula cha jioni baada ya mchezo huo ili pamoja na wachezaji siku hiyo.
  Naye Rais wa Yanga SC, Hersi Said alimkabidhi RC Chalamila jezi ya kijani ya timu hiyo aivae siku ya Jumapili.


  Mchezo huo utachezeshwa na refa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jean-Jacques Ngambo Ndala atakayesaidiwa na Mkongo mwenzake, Olivier Kabene Safar na Zakhele Thusi Granville Siwela wa Afrika Kusini watakaokuwa wanakimbia na vibendera pembezoni mwa Uwanja kulia na kushoto.
  Mchezo wa marudiano utafuatia Juni 3 Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers nchini Algeria na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) litatoa orodha nyingine ya waamuzi.
  Kufika hatua hii, Yanga imeitoa Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1, ikishinda 2-0 nyumbani na 2-1 ugenini, wakati USM Alger imeitoa ASEC Mimosas ya Ivory Coast baada ya sare ya 0-0 ugenini na ushindi wa 2-0 nyumbani. 


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MKUU MPYA WA MKOA DAR ANUNUA TIKETI 1,000 YANGA NA USM ALGER Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top