• HABARI MPYA

    Thursday, May 11, 2023

    HONGERA YANGA SC, KILA LA HERI KWENYE MCHEZO WA MARUDIANO


    MABINGWA wa Tanzania, Yanga SC jana walibisha hodi Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
    Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, vijana wa kocha Mtunisia, Nasredeen Nabi wakaimaliza Marumo Gallants kipindi cha pili kwa mabao ya viungo marafiki, Mburkinabe Stephane Aziz Ki dakika ya 64 na Mghana Bernard Morrison dakika ya 90 na ushei.
    Sasa Yanga SC wanatakiwa kwenda kuulinda ushindi huo kwenye mchezo ww marudiano Mei 17 Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng, NW.
    Wakifanikiwa kuitoa Marumo Gallants, katika Fainali zitakazopigwa Mei 28 na Juni 3, Yanga watakutana na mshindi wa jumla kati ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast na USM Alger ya Algeria ambazo jana zilitoka sare ya 0-0 Abdidjan. 
    Mara tu baada ya mchezo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan aliwapongeza Yanga SC kwa ushindi huo na kuwatakia kilala heri kwenye mchezo wa marudiano nchini Afrika Kusini wiki ijayo.
    “Hongereni Yanga kwa ushindi katika mchezo wenu wa raundi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup). Nawatakia maandalizi mema kwa mchezo wenu wa raundi ya pili, muendelee kuiheshimisha nchi yetu. Hamasa yangu inaendelea,” amesema Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
    Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Yanga kucheza Nusu Fainali ya michuano yoyote ya Afrika baada ya kukomea Robo Fainali mara nne awali, mara tatu katika Ligi ya Mabingwa 1969, 1970 na 1998 na mara moja katika Kombe la Washindi 1995. 
    Mwaka 1974 Simba iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika Nusu Fainali ya Michuano ya Afrika, ilikuwa klabu bingwa Afrika ilipoitoa Hearts Of Oak ya Ghana kwa ushindi wa 2-1 Accrah mabao ya Adamu Sabu (marehemu) na Abdallah Kibadeni na sare ya 0-0 Dar es Salaam.
    Simba ikaenda kutolewa Ghazl El Mahalla ya Misri kwa penalti 3-0 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0, bao la Wekundu wa Msimbazi hapa Dar es Salaam likifungwa na Saad Ally.
    Mwaka 1993 Simba ikaandika historia ambayo bado haijavunjwa, kufika Fainali ya Kombe la CAF kufuatia kuwatoa  Atlético Sport Aviação (ASA) kwa mabao 3-1 Dar es Salaam na sare ya 0-0 Jijini Luanda, Angola – na kwenye Fainali ikafungwa 2-0 na Stella Adjamé ya Ivory Coast hapa hapa Dar es Salaam ikitoka kutoa sare ya 0-0 Abidjan.
    Mwaka 1995 Malindi ya Zanzibar nayo ikafika Nusu Fainali ya Kombe la CAF kufuatia kuitoa OC Agaza ya Togo kwa ushindi wa 2-0 ugenini pia kufuatia sare ya 0-0 Zanzibar na yenyewe ikaenda kutolewa na Etoile du Sahel ya Tunisia kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 kwake.
    Mwaka 2003 Simba wakafika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 kwake.
    Kama ilivyokuwa mwaka 1998, Robo Fainali za 2003 pia zilichezwa kwa mtindo wa makundi ambao sasa umebadilishwa makundi ni 16 Bora.
    Miaka 30 tangu Simba iicheze Fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kufungwa na Stella Adjame 2-0 hapa Dar es Salaam kufuatia sare ya 0-0 Ivory Coast, klabu nyingine ya Tanzania, Yanga inatarajiwa kwenda kuivunja rekodi hiyo na kujaribu kuweka mpya – kuwa klabu ya kwanza nchini kutwaa Kikombe cha Afrika.
    Yanga wanahitaji kujipanga vyema kwa mechi hiyo ya marudiano dhidi ya Marumo Gallants wakacheze kwa nidhamu ya hali juu Mei 17 ili kuulinda ushindi wao wa nyumbani na hatimaye kukata tiketi ya Fainali. 
    Hakuna kinachoshindikana chini ya jua, kama wamefika Nusu Fainali, wanaweza kufika Fainali na kubeba Kombe pia.
    Hongera Yanga kwa ushindi wa jana chini ya kocha mtaalamu kabisa Nasredine Mohamed Nabi raia wa Tunisia, na kama alivyosema Mheshimiwa Rais Dk. Samia, mmeiheshimisha nchi. Kila la heri katika mchezo wa marudiano wiki ijayo.
    Tunatarajia kuona Fainali ya Kombe CAF inachezwa hapa Dar es Salaam. Mungu aendelee kuwasimamia Mashujaa wetu. Kila la heri Yanga Afrika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HONGERA YANGA SC, KILA LA HERI KWENYE MCHEZO WA MARUDIANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top