• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 05, 2020

  TANZANIA PRISONS WAICHOMOLEA AZAM FC DAKIKA YA MWISHO, ZATOKA SARE YA 1-1 UHURU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Lakin Azam FC watajilaumu wenyewe kwa sare hiyo ambayo inawafanya wafikishe pointi 38 katika mchezo wa 19, sasa wakizidiwa ponti 12 na vinara, Simba SC kwani baada ya kuongoza kwa muda mrefu mchezo huo, wakawaruhusu wageni kusawazisha katika dakika ya mwisho ya muda wa fidia baada ya muda wa kawaida. 
  Azam FC inayofundishwa na kocha Mromania, Aristica Cioaba iliuanza vizuri mchezo na kufanikiwa kwenda mapumziko ikiwa inaongoza 1-0 kwa bao la mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 45 akimalizia pasi ya beki Mzimbabwe, Bruce Kangwa.


  Na hata kipindi cha pili, Azam FC walirejea vizuri na kucheza kwa umakini wakijilinda zaidi na kushambulia kwa kushitukiza.
  Mchezo ulisimama kwa dakika tatu kuanzia ya 79 baada ya refa Jeonisia Rukyaa kumuamuru kipa Mghana, Razack Abalora aende kubadilisha moja ya nguo zake iliyokuwa imechanika.
  Na aliporejea upepo ukabadilika kidogo, Tanzania Prisons wakawa wanepeleka mashambulizi ya nguvu langoni mwa Azam, ambayo yalizaa matunda dakika ya 90 na ushei baada ya Jumanne Elfadhili kufunga bao la kusawazisha akimalizia kwa kichwa kona ya Cleophace Mkandala.
  Lakini pamoja na kipa Abalora kuokoa mpira huo ukiwa unaelekea nyavuni na kurudi uwanjani – refa Jeonesia Rukyaa alimuamuru mwanamama mwenzake wanayetoka naye mkoani Kagera, Grace Wamara kurudi katikati wakati wachezaji wa Azam FC wakiendelea kupinga uamuzi huo.
  Hata hivyo, baada ya dakika moja, wachezaji hao wa Azam FC wakakubali kuanza tena mchezo huo kabla ya Jeonesia kupuliza kipyenga cha mwisho sekunde chache zilizofuatia. 
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Nico Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohamed, Aggrey Morris, Bryson Raphael, Iddi Suleiman ‘Nado’, Frank Domayo/Never Tigere dk60, Obrey Chirwa/Osca Masai dk89, Richard Ella D’jodi/Andrew Simchimba dk76 na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
  Tanzania Prisons; Jeremiah Kisubi, Michael Ismail, Benjamin Asukile, Nurdin Chona/Cleophace Mkandala dk63, Vedastus Mwihambi, Jumanne Elfadhil, Salum Kimenya, Hamidu Mohamed, Freddy Chudu/Samson Mbagula dk40, Jeremiah Juma na Ismail Aziz/Ezekieli Mwashilindi dk36. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo; Bao pekee la Charles Ilanfya dakika ya 86 lilitosha kuipa ushindi wa ugenini wa 1-0 KMC dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  Na Ruvu Shooting ikaichapa 1-0 Mtibwa Sugar, bao pekee Fully Maganga dakika ya 75 Uwanja wa Mabatini, Mlandzi mkoani Pwani.
  Na Ndanda SC ikaibuka na ushindi mnono wa 3-0 dhidi ya Mbao FC, mabao ya Vitalisy Mayanga dakika ya tatu na mkongwe Hussein Javu dakika ya 68 na 88 Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
  Namungo FC ikalazmishwa sare ya 1-1 na Alliance FC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, wenyeji hao wakitangulia kwa bao la Reliants Lusajo dakika ya 33, kabla ya Zabona Hamisi kuwasawazishia wageni dakika ya 77.
  Biashara United wakaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Singida United Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara mabao yao yote yakifungwa na Innocent Edwin dakika ya 18 na 54 na la wageni likifungwa Mtilika Said dakika ya 44.
  Nayo Kagera Sugar ikaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mwadui FC, mabao yake yakifungwa na Yusuph Mhilu dakika ya 15 na Kelvin Kongwe Sabato dakika ya 38, huku la wageni likifungwa na Omary Daga dakika ya 45.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TANZANIA PRISONS WAICHOMOLEA AZAM FC DAKIKA YA MWISHO, ZATOKA SARE YA 1-1 UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top