• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 16, 2020

  SAMATTA ASABABISHA BAO LA KWANZA, LAKINI ASTON VILLA YACHAPWA TENA 3-2 NA TOTTENHAM

  Na Mwandishi Wetu, BIRMINGHAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesababisha bao la kwanza la Aston Villa ikichapwa 3-2 na Tottenham Hotspur katika mchezo wa Ligi Kuu ya England leo Uwanja wa Villa Park.
  Samatta aliirukia krosi ya kiungo Mholanzi, Anwar El Ghazi kujaribu kuunganishia nyavuni, lakini beki Mbelgiji Toby Alderweireld akaiwahi kujaribu kuokoa kwa bahati mbaya akajifunga kuwapa Villa bao la kuongoza dakika ya tisa tu.
  Alderweireld akaisawazishia Spurs dakika ya 27, kabla ya refa Martin Atkinson kutumia msaada wa Teknolojia ya Video (VAR) kuwapa Tottenham penalti mwishoni mwa kipindi cha kwanza kufuatia Bjorn Engels kumuangusha Steven Bergwijn.
  Mbwana Samatta amesababisha Toby Alderweireld ajifunge kuipatia Aston Villa bao la kwanza la leo Uwanja wa Villa Park 

  Son Heung-min akaenda kupiga penalti iliyookolewa na kipa Pepe Reina, lakini akauwahi mpra na kuukwamisha nyavuni dakika ya 45 kabla ya kufunga na bao la ushindi dakika ya 90 na ushei kufuatia Bjorn Engels kuisawazishia Villa dakika ya 53.
  Samatta aliyejiunga na Villa katikati ya mwezi uliopita akitokea KRC Genk ya Ubelgiji, klabu yake ya kwanza Ulaya iliyomnunua Januari mwaka 2016 kutoka TP Mazembe ya Jamhuri ya Kodemokrasia ya KOngo (DRC) alipumzishwa dakika ya 83 nafasi yake ikichukuliwa na Mspaniola, Borja Baston.
  Leo Samatta amecheza mechi ya pili ya EPL baada ya kufunga bao moja Aston Villa ikichapwa 2-1 na wenyeji, AFC Bournemouth Februari 1 kwenye mchezo uliopita Uwanja wa Vitality. 
  Samatta pia alicheza mechi ya marudiano ya Nusu Fainali ya Kombe la Ligi England, Aston Villa ikiichapa Leicester City 2-1 Januari 28 na kutinga fainali ambako sasa itamenyana na Manchester City Machi 1 Uwanja wa Wembley 
  Matokeo ya leo si mazuri kwa Aston Villa inayofundishwa na kocha Muingereza, Dean Smith kwani inabaki na pointi zake 25 baada ya kucheza mechi 26 ikibaki nafasi ya 17 katika ligi ya timu 20 ambayo mwisho mwa msimu timu tatu zitateremka.
  Kwa Spurs ya kocha Mreno, Jose Mourinho baada ya ushindi huo inafikisha pointi 40 katika mchezo wa 26 pia na kupanda kwa nafasi moja hadi ya tano, ikiishusha Sheffield United yenye pointi 39 za mechi 29.
  Liverpool inaendelea kuongoza Ligi Kuu England kwa pointi zake 76 za mechi 26 ikifuatiwa na Manchester City yenye pointi 51 za mechi 25, Leicester City pointi 50 za mechi 26 na Chelsea yenye pointi 41 za mechi 25.
  Kikosi cha Aston Villa kilikuwa: Reina, Konsa, Engels, Hause, Guilbert, Drinkwater/Nakamba dk60, Luiz, Targett, El Ghazi/Trezeguet dk70, Samatta/Baston dk83 na Grealish.
  Tottenham Hotspur: Lloris, Aurier, Sanchez, Alderweireld, Davies, Winks, Dier/Lo Celso dk60, Moura, Alli/Fernandes dk83, Bergwijn/Vertonghen dk90+4 na Son.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA ASABABISHA BAO LA KWANZA, LAKINI ASTON VILLA YACHAPWA TENA 3-2 NA TOTTENHAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top