• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 22, 2020

  SIMBA SC YAICHAPA BIASHARA 3-1 NA KUZIDI KUUKARIBIA UBINGWA WA TATU MFULULIZO LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wameendeleza wimbi la ushindi katika kampeni yao ya kutwaa taji la tatu mfululizo baada ya kuwachapa Biashara United ya Mara mabao 3-1 usiku wa leo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo uliotokana na mabao ya wachezaji wa kigeni watupu, Luis Miquissone kutoka Msumbiji, Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere na Mkenya Fransic Kahata, Simba SC inatanua uongozu wake katika Ligi Kuu kwa pointi 17 zaidi ya Azam FC wanaofuatia nafasi ya pili.
  Simba SC inayofundishwa na Mbelgiji, Sven Ludwig Vandonbroeck anayesaidiwa na wazalendo, Suleiman Matola, kocha wa makipa Muharami Mohamed ‘Shilton’ na kocha wa Fiziki, Mtunisia, Adel Zrane inafikisha pointi 62, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 45 baada ya wote kucheza mechi 24.
  Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Abdallah Mwinymkuu aliyesadiwa na Abdallah Rashid na Credo Mbuya dalili za SImba SC kupata ushindi mzuri zilianza mapema tu baada ya mshambuliaji wake, Meddie Kagere kukosa penalti dakika ya 26.
  Penalti hiyo ilitolewa baada yeye mwenyewe, Kagere kusukumwa na Derick Mussa kwenye boksi na sifa zimuendee kipa Daniel Mgore aliyepangua shuti la Meddie na kabla ya kuurukia tena mpira na kuudaka kuinyima bao la mapema Simba SC.
  Lakini mchezaji mpya, Luis Miquissone akaifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya 35 akimalizia pasi nzuri ya kiungo Jonas Gerlad Mkude.
  Kiungo Miquissone akatia krosi moja nzuri iliyokuwa inaelekea nyavuni, lakini Kagere akaenda kuisindikiza langoni mwa Biashara kuipatia Simba SC bao la pili dakika ya 69, kabla ya Novarty Dismas kuifungia Biashara United dakika ya 71 akimalizia pasi ya Atupele Green. 
  Mchezaji mwingine mpya, Francis Kahata akakamilisha shangwe za mabao Simba SC kwa kufunga bao la tatu dakika ya 88 akimalizia pasi ya kiungo mwenzake, Mzambia Clatous Chama
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Clatous Chama, Lus Miquissone/Hassan Dilunga dk90, Meddie Kagere/Sharaf Eldin Shiboub dk80, John Bocco/Kennedy Juma dk90+2 na Francis Kahata.
  Biashara United; Daniel Mgore, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Innocent Edwin/Jerome Lambele dk82, Novatus Dismas, Wilfred Kourouma/Ally Kombo dk47, Atupele Green, Derick Mussa, James Mwasote, Abdulmajid Mangaro, Baraka Nyakamande/Okorie Milton dk47 na Justine Omary.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAICHAPA BIASHARA 3-1 NA KUZIDI KUUKARIBIA UBINGWA WA TATU MFULULIZO LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top