• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 15, 2020

  ‘KAPTENI’ JOHN BOCCO APIGA BAO PEKEE UWANJA WA SAMORA SIMBA SC YAWALAZA LIPULI FC 1-0

  Na Mwandishi Wetu, IRINGA
  BAO pekee la Nahodha John Rapahel Bocco limetosha kuifanya Simba SC iendeleze wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwachapa wenyeji, Lipuli FC 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  Bocco, mshambuliaji wa zamani wa Azam FC alifunga bao hilo dakika ya 26 akimalizia pasi ya kiungo wa kimataifa wa Kenya, Francis Kahata Nyambura.
  Na kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na Mbelgiji, Sven Ludwig Vandonbroeck anayesaidiwa na wazalendo, Suleiman Matola, kocha wa makipa Muharami Mohamed ‘Shilton’ na kocha wa Fiziki, Mtunisia, Adel Zrane inafikisha pointi 56 katika mchezo wa 22.


  Maana yake Simba SC inazidi kutanua uongozi wake katika Ligi Kuu hadi pointi 12 zaidi ya Azam FC ambayo leo imechapwa 2-1 na Coastal Union Jijini Dar es Salaam.
  Mabao ya Coastal Union jioni ya leo Uwanja wa Uhuru yamefungwa na Ayoub Lyanga dakika ya 37 na Mudathir Said dakika ya 64, wakati bao pekee la Azam FC limefungwa na mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 90 na ushei.
  Sasa Coastal Union inafikisha pointi 38 katika mchezo wa 22 na kurejea nafasi ya tatu, ikiishusha Yanga ambayo usiku wa leo inamenyana na Tanzania Prisons Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam pia. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Ruvu Shooting imeichapa 1-0 Mbeya City bao pekee la Fully Maganga dakika ya 50 Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. 
  Biashara United pia imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Alliance bao pekee la Okorie James dakika ya 45 na ushei Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
  Ndanda FC imeibuka na ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya Singida United, bao pekee la Vitalisy Mayanga dakika ya 80 Uwanja wa Liti, Sngida.
  JKT Tanzania imeibuka na ushindi wa ugenini wa 1-0 pia dhidi ya Mtibwa Sugar, bao pekee la Danny Lyanga dakika ya 33 kwa penalti.
  Mwadui FC imetoka nyuma na kupata sare ya ya 1-1 nyumbani na Namungo FC Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga. Namungo ilitangulia kwa bao la Nzigamasabo Steve dakika ya nane kabla ya Raphael Aloba kuisawazishia Mwadui dakika ya 49.
  Nayo Kagera Sugar imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbao FC, mabao yake yakifungwa na Geoffrey Mwashiuya dakika ya nane na Yusuph Mhilu dakika ya 31 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Polisi Tanzania imeibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya wenyeji, Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, mabao yake yakifungwa na Marcel Kaheza dakika ya 10, Matheo Anthony dakika ya 39 na Baraka Majogoro dakika ya 87 – na ya wenyeji yakifungwa na Abdul Hillary dakika ya 80 na Ally Ramadhani dakika ya 83.
  Kikosi cha Lipuli FC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, David Kameta, Paul Ngalema, Peter Mwangosi, Novart Lufunga, David Majinge, Mwinyi Ahmed, Freddy Tangalo, Joshua Ibrahim/Said Mussa dk85, Daruwesh Saliboko na Keneth Masumbuko/Issa Ngoah dk66.
  Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/luis miquisone dk83, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco na Francis Kahata.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ‘KAPTENI’ JOHN BOCCO APIGA BAO PEKEE UWANJA WA SAMORA SIMBA SC YAWALAZA LIPULI FC 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top