• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 23, 2020

  YANGA SC YAZIDI KUPOTEZA MATUMAINI YA UBINGWA BAADA YA SARE NYINGINE LEO MKWAKWANI

  Na Mwandishi Wetu, TANGA
  NDOTO za ubingwa zimezidi kuyeyuka kwa vigogo, Yanga SC baada ya leo kulazimishwa sare ya nne mfululizo kufuatia kutoka 0-0 na wenyeji, Coastal Union Uwanja Mkwakwani, Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Ni sare ya pili mfululizo ugenini, wakitoka kutoa sare ya 1-1 na Polisi Tanzania Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya sare nyingine mbili mfululizo nyumbani, 1-1 na Mbeya City na 0-0 na Tanzania Prisons Uwanja wa Taifa.
  Kwa sare hiyo, Yanga SC inafikisha pointi 41 baada ya kucheza mechi 22, ikibaki nafasi ya nne nyuma ya Namungo FC yenye pointi 43 za mechi 23 na Azam FC yenye pointi 45 za mechi 24, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wanaendelea kuongoza kwa pointi zao 62 za mechi 24.

  Kocha Mbelgiji, Luc Aymael leo hakuwachezesha washambuliaji wote wa kigeni, David Molinga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Muiviry Coast, Yikpe Gislain – badala yake akawaanzisha wazawa Tariq Seif na Ditram Nchimbi ambao hata hivyo hawakufurukuta mbeke ya safu ya ulinzi ya Coastal.
  Yanga SC imeendelea kucheza vizuri nje ya eneo la hatari la wapinzani, lakini pia imeendelea kukosa mipango ya kutengeneza nafasi za mabao badala yake inacheza kulazimisha – ingawa makosa ya safi ya ulinzi yameendelea kupungua.  
  Kikosi cha Coastal Union kilikuwa; Soud Abdallah, Hassan Kibailo, Hance Masoud, Ibrahim Ame, Bakari Mwamnyeto, Salum Ally, Mtenje Albano, Ayoub Semvua, Mudathir Said, Ayoub Lyanga na Issa Said.
  Yanga SC; Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Abdulrahman, Said Juma ‘Makapu’, Lamine Moro, Papy Kabamba Tshishimbi, Mapinduzi Balama/Mrisho Ngassa, Haruna Niyonzima/Erick Kabamba, Ditram Nchimbi, Tariq Seif/Ally Mtoni ‘Sonso’ na Bernard Morrison.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAZIDI KUPOTEZA MATUMAINI YA UBINGWA BAADA YA SARE NYINGINE LEO MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top