• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 22, 2020

  KOCHA ATOZWA FAINI SH 200,000 NA KUFUNGIWA MWEZI KWA KUMTUKANA REFA DARAJA LA PILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa makipa wa timu ya Eagle FC, Greyson Mwanjombewa ametozwa faini ya Tsh 200,000 na kufungiwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kwa kosa la kumtukana mwamuzi wa akiba timu yake ikishinda 2-0 dhidi ya Rufiji FC Februari 3 Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
  Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(2) kuhusu Udhibiti wa Viongozi. Nayo Mkamba Rangers imetozwa faini ya Tsh 50,000 kwa kosa la kutofika katika kikao cha maandalizi ya mchezo (Pre match meeting) katika mchezo ambao walifungwa 3-1 na Rufiji FC Februari 10 Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
  Adhabu imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 14 (2) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo. Timu za Mpwapwa FC na Rufiji FC zote zimepewa Onyo kali kwa kitendo cha kutomaliza mchezo baina yao kwa kisingizio cha mvua kuwa kubwa na vurugu za Februari 15 Uwanja wa Mgambo mkoani Dodoma. Mechi hiyo ilimaliziwa Februari 16 na Mpwapwa FC wakaibuka na ushindi wa 1-0.
  Aidha, Mpwapwa FC imepewa Onyo kwa kosa la mashabiki wake kumtolea matusi mwamuzi kwa kutaka mchezo uendelee hata kama uwanja haukidhi vigezo kwa wakati huo kwenye mchezo uliofanyika Februari 15, 2020 na kulazimika kumaliziwa Februari 16, 2020 uwanja wa Mgambo mkoani Dodoma.
  Kiongozi wa timu ya Mpwapwa FC Omary Mustafa anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kwa kosa la kuanzisha fujo kwa kuingia kwenye vyumba vya waamuzi na kutoa lugha za matusi na kejeli kwa waamuzi katika mchezo uliofanyika Februari 15, 2020 uwanja wa Mgambo Dodoma.
  Nayo Mgambo Shooting FC imetozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la mashabiki wake kumvamia na kuanza kumpiga ngumi mwamuzi Abdu Kalenzo kwenye mchezo dhidi ya Milambo FC walioshinda 2-1 Februari 17 Uwanja wa St. Vicent mkoani Tabora.
  Adhabu imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 43 (1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa klabu. Aidha, Mgambo FC imepewa Onyo Kali kwa kitendo cha viongozi wao kutofika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (Pre match meeting) katika mchezo uliofanyika Februari 17, 2020 uwanja wa St. Vicent mkoani Tabora.
  Adhabu imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 14 ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KOCHA ATOZWA FAINI SH 200,000 NA KUFUNGIWA MWEZI KWA KUMTUKANA REFA DARAJA LA PILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top