• HABARI MPYA

    Sunday, February 16, 2020

    TWIGA STARS YAENDELEA KUNG'ARA MICHUANO YA TUNISIA, YAWACHAPA ALGERIA 3-2

    Na Somoe Ng'itu, TUNIS
    TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake ( Twiga Stars) imeendelea kufanya vizuri katika mashindano ya Kombe la UNAF baada ya kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Algeria katika mchezo uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Kram jijini Tunis nchini hapa.
    Kwa ushindi huo, Twiga Stars imefikisha pointi sita na kuongoza katika msimamo wa mashindano hayo yanayoshirikisha nchi tano za Kanda ya Kaskazini na Tanzania wakiwa wageni waalikwa.
    Bao la kwanza la Twiga Stars lilifungwa na Mwanahamisi Omary "Gaucho" katika dakika ya 11 na dakika ya 22 Algeria walisawazisha kupia Dellidj Anissa.

    Dakika ya 44 Affak Horiya aliifungia Algeria bao la pili na sekunde chache kabla ya kwenda mapumziko, Gaucho, mshambuliaji wa Simba Queens aliisawazishia Twiga Stars kwa kufunga bao la pili.
    Diana Msewa aliwanyanyua mashabiki wa Twiga Stars baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya lala salama na kuipa timu yake pointi tatu muhimu.
    Kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana kusaka ushindi katika mchezo huo wa pili mfululizo.
    "Kila timu inavyocheza inazidi kuimarika, kuna makosa yapo tumeyabaini, tutayarekebisha kwa ajili ya mechi inayofuata, tunaendelea kujifunza na kuwapa uzoefu wachezaji wetu kupitia michuano kama hii, inawaimarisha kwa ajili ya mechi za mashindano," alisema Shime.
    Twiga Stars itashuka tena dimbani keshokutwa kucheza dhidi ya Morocco ambayo nayo iliwafunga Tunisia katika mchezo wa kwanza na itamaliza dhidi ya wenyeji hao Februari 22, mwaka huu.
    Jana jioni Tunisia ilishuka dimbani kuwakaribisha Mauritania, timu zote zikiwa na kumbukumbu ya kufungwa katika mechi zao za kwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TWIGA STARS YAENDELEA KUNG'ARA MICHUANO YA TUNISIA, YAWACHAPA ALGERIA 3-2 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top