• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 08, 2020

  MOLINGA ‘FALCAO’ AING’ARISHA YANGA SC LIGI KUU, YAICHAPA RUVU SHOOTING 1-0 UHURU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), David Molinga Ndama ‘Falcao’ dakika ya 39 akimalizia kwa kichwa krosi maridadi ya Ditram Nchimbi kutoka kulia.
  Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 37 baada ya kucheza mechi 18, ingawa inabaki nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye point 41 sasa baada ya kucheza mechi 20 na mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 50 za mechi 20 pia.


  Yanga SC nayofundishwa na Mbelgiji Luc Aymael anayesaidiwa na mzawa, Charles Boniface Mkwasa, kocha wa Fiziki, Riedoh Berdien kutoka Afrika Kusini na kipa wa zamani wa klabu, Manyika Peter anayewanoa walinda milango wa timu hiyo wangeweza kuondoka na ushindi mnono zadi kama wangetumia vyema nafasi nzuri walizotengeneza.
  Sifa zimuendee kipa Mohamed Makaka  wa Ruvu Shooting kwa kuokoa michomo mingine miwili ya Molinda kipindi cha kwanza na mmoja wa Muivory Coast, Yikpe Gislain aliyetokea benchi kipindi cha pili.
  Dakika ya 31 Yanga walilalamika kunyimwa penalti baada ya Baraka Mtuwi kumchezea rafu mchezaji wao, Mghana Bernard Morrison kwenye boksi aliyekuwa amefanikiwa kumtoka beki mwingine wa Ruvu Shooting, Kassim Simaulanga upande wa kulia.
  Kikosi cha Ruvu Shooting kilikuwa; Mohamed Makaka, Omary Kindamba, Kassim Simbaulanga, Santos Mazengo, Baraka Mtuwi, Zubery Dabi, William Patrick/Shaaban Msala dk58, Shaaban Kisiga, Fully Maganga, Graham Naftali/Saadat Mohamed dk60 na Abdulrahman Mussa/Jamal Mnyante dk62.
  Yanga SC; Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohamed, Lamine Moro, Ally Mtoni, Papy Kabamba Tshishimbi, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzma/ Said Juma ‘Makapu’ dk90, David Molinga/ Yikpe Gislain dk69, Mapinduzi Balama na Bernard Morrison/Deus Kaseke dk81. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Azam FC imeibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya KMC Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, mabao yake yakifungwa na washambuliaji Muivory Coast, Richard D’jodi dakika ya 25 na Mzambia Obrey Chirwa mawili dakika ya 33 na 43, huku bao pekee la wapinzani wao likifungwa na Sadallah Lipangile dakika ya 84.
  Coastal Union ikaibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania mabao ya Mtenje Albano dakika ya 69 na Mudathir Said dakika ya 90 Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
  Bao pekee la Mwinyi Elias dakika ya 20 likatosha kuipa Lipuli FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Gairo, Morogoro. 
  Nayo Mbeya City ikaibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya mahasimu wao wa Jiji, Tanzana Prisons bao pekee la Peter Mapunda kwa penalti dakika ya 13 Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  Bao la dakika ya 65 la Sameer Vincent likaisaidia Alliance FC kupata sare ya 1-1 na Mbao FC iliyotangulia kwa bao la Datius Peter dakika ya 55 kwa penalti Uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.
  Singida United nayo ikalazimishwa sare ya 2-2 na Mwadui FC Uwanja wa Liti, SIngida. Mabao ya Singida yalifungwa na Muharami Issa ‘Marcelo’ dakia ya 61 na 90 na ya Mwadui FC yalifungwa na Venance Ludovic dakika ya 24 na Raphael dakika ya 41.
  Ndanda SC ikalazimishwa sare ya 0-0 na Namungo FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Kagera Sugar nao wakalazimishwa sare ya 0-0 na Biashara United Uwanja wa Kaitaba mjin Bukoba.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MOLINGA ‘FALCAO’ AING’ARISHA YANGA SC LIGI KUU, YAICHAPA RUVU SHOOTING 1-0 UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top