• HABARI MPYA

    Sunday, January 05, 2020

    SARE NA YANGA JANA; SIMBA SC YALIA NA WACHEZAJI WAKE KUTOJITUMA KAMA WAPINZANI WAO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSEMAJI wa Klabu ya Simba SC Haji Manara amewataka wachezaji wa timu hiyo kutambua thamani ya jezi yao na kujituma zaidi wawapo uwanjani kama wafanyavyo wapinzani wao wa jadi Yanga.
    Manara ametoa ujumbe huo ikiwa ni siku moja baada ya Simba kulazimishwa sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa jana, akisema kuwa kuna baadhi ya wachezaji ‘waliboa’ jambo linalowapa Yanga jeuri ya kutamba mitaani.
    “Wenzenu hawapati mnachokipata, wanapanda daladala hadi Mbeya, hawakai camp nzuri, hawalipwi kwa wakati, hawapati bonus mzipatazo lakini wanawazidi fighting spirit na commitment kwa mbali sana!!.... Kifupi baadhi yenu mmeboa mno!!” amesema Manara kupitia mtandao wa Instagram. 
    Ameongeza kuwa kwa mchezao wa jana, Simba haikustahili matokeo ya sare, huku akiwabebesha lawama wachezaji kwamba wamewaangusha mashabiki, uongozi na bodi ya wakurugenzi chini ya mwenyekiti wake Mohamed Dewji.
    Simba SC jana ililazimishwa sare ya 2-2 na watani wa jadi, Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Kwa sare hiyo, Simba SC inafikisha pointi 35 katika mchezo wa 14, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 10 zaidi ya mahasimu wao hao wa jadi, ambao hata hivyo wamecheza mechi 12 tu.
    Katika mchezo huo, mabingwa watetezi Simba SC ndiyo walioanza kupata kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere dakika ya 42 kwa penalti ya utata iliyotolewa na refa Jeonisia Rukyaa baada ya beki wa Yanga, Kelvin Yondan kumvuta kwa mkopo Mnyarwanda huyo nje kidogo ye boksi, lakini akaenda kuangukia ndani.
    Dakika ya kwanza tu baada ya kuanza kipindi cha pili Simba SC wakafanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa kiungo Deogratius Kanda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akimalizia pasi ya Kagere.
    Kiungo mpya, Balama Mapinduzi akaifungia Yanga SC bao la kwanza kwa shuti la umbali wa mita 30 baada ya kumpokonya mpira kiungo wa wapinzani, Muzamil Yassin dakika ya 49.
    Wakati Simba bado wanajiuliza, Yanga SC wakafanikiwa kusawazisha bao la pili kupitia kwa kiungo wake, Mohamed Issa ‘Banka’ dakika ya 53 akimalizia kwa kichwa krosi ya beki wa kushoto, Adeyoum Ahmed.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SARE NA YANGA JANA; SIMBA SC YALIA NA WACHEZAJI WAKE KUTOJITUMA KAMA WAPINZANI WAO Rating: 5 Reviewed By: Mwakasege Blog
    Scroll to Top