• HABARI MPYA

  Jumamosi, Oktoba 05, 2019

  NAHODHA WA KIKOSI CHA NIGERIA OLIMPIKI YA BEIJING AFARIKI DUNIA MAREKANI

  NYOTA wa zamani wa Olimpiki wa Nigeria, Isaac Promise alifariki dunia Alhamisi (Oktoba 3, 2019) nchini Marekani akiwa ana umri wa miaka 31, klabu yake Austin Bold imesema.
  “Austin Bold FC inasikitika kutangaza kifo cha Promise Isaac aliyefariki dunia usiku wa Jumatano akiwa ana umri wa miaka 31. Mawazo yetu yapo pamoja na familia yake, rafiki zake na wachezaji wenzake,” imesema taarifa ya klabu. 
  Nalo Shirikisho la Soka Nigeria (NFF) limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo; “Tumepokea kwa majonzi taarifa za kifo cha mshambuliaji wa zamani wa Super Eagles, Isaac Promise. Promise alikuwa Nahodha wa Eagles kwenye Olimpiki ya Beijing kilichoshinda Medali ya Fedha. Mawazo yetu na wachezaji yapo pamoja na familia yake kwa sasa,”.
  Nahodha wa kikosi cha Nigeria cha Olimpiki ya Beijing, Isaac Promise amefariki dunia akiwa ana umri wa miaka 31

  Promise atakumbukwa zaidi kwa umahiri wake alipokuwa anachezea timu za vijana za Nigeria kuanzia chini ya miaka 20 na kikosi cha Olimpiki.
  Alikuwa Nahodha wa kikosi cha Nigeria kilichotwaa ubingwa wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za U-20 (wakati ikijulikana Ubingwa wa Vijana Afrika) mwaka 2005 nchini Benin,akifunga mabao yote katika fainali dhidi ya Misri. 
  Baadaye mwaka huo, aliiongoza Flying Eagles kufika fainali ya Kombe la Dunia la Vijana ambako walifungwa 2-1 na Argentina.
  Mwaka 2008, akaifikisha tena Nigeria fainali ya Michezo ya Olimpiki mjini Beijing, wakifungwa tena  na Argentina.
  Kwa muda mrefu alicheza Uturuki, klabu za Genclerbirligi, Trabzonspor, Manisaspor, Antalyaspor, Balikesirspor, Karabjuspor na Giresunspor kabla ya kuhamia Marekani mwaka 2018 alipojiunga na Georgia Revolution kabla ya kuhamia Austin Bold msimu huu, 2019, akichezea timu hiyo ya Daraja la Kwanza hadi kifo chake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NAHODHA WA KIKOSI CHA NIGERIA OLIMPIKI YA BEIJING AFARIKI DUNIA MAREKANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top