• HABARI MPYA

    Saturday, April 07, 2018

    WAMBURA AJIPANGA KUPAMBANA NA TFF KIVINGINE…ASEMA ATAKULA NAO SAHANI MOJA HADI KIELEWEKE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura amesema kwamba amejipa muda na mawakili wake hadi Jumatatu kutafakari pa kwenda kupata haki yao.
    Wambura ameyasema hayo katika Mkutano wake na Waandishi wa Habari ukumbi wa Break Point, Dar es Salaam leo kufuatia jana Kamati ya Rufaa ya Maadili kuitupa rufaa yake ya kupinga kufungiwa maisha na Kamati ya Maadili ya TFF.
    “Nimesikitishwa na hukumu iliyotolewa jana, kwa sababu kwanza haikujilekeza kwenye rufaa yenyewe, imejielekza kwenye mambo ya nje ya rufaa. Wakati wa kikao cha Kamati ya Rufaa, TFF hawakujibu kitu, labda kama walikaa na Kamati pembeni,”amesema Wambura.

    Michael Wambura (kulia) akiziungumza na Waandishi wa Habari leo ukumbi wa Break Point, Dar es Salaam 

    Wambura amesema kwamba kinamchomsikitisha zaidi ni kitendo cha Mwenyekiti wa Kamati Rufaa ya Maadili, Ebenezer Mshana kuukataa ukweli kwa lazima kuhusu muundo wa Kamati ya Maadili ya TFF na viongozi wake.
    “Baya kuliko yote, ni pale ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa (Ebenezer Mshana) anapoamua kusema mambo ambayo hayakuzungumzwa kwenye kikao ha rufaa. Ila kwa kuwa wao wamefanya maamuzi na wapo kwenye Uwanja wa nyumbani, sisi acha tusonge mbele,”amesema.
    Lakini Wambura amesema kwamba inawawia vigumu kwenda Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (CAS) ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa sababu ya kanuni ya Maadili ya TFF Ibara ya 74.4, ambayo inasema; “Maamuzi ya kamati ya Rufaa yatakuwa ni mwisho na hayatajadailiwa na chombo kingine chochote,”.
    Wambura amesema na sheria ya 48 ya CAS kuhusu rufaa inaagiza kwamba anayepeleka Rufaa CAS aambatanishe na kipengele cha sharia cha shirikisho la nchi yake, kinachomruhusu kwenda huko.
    “Lakini sasa huku tayari Kanuni ya 74.4 ya Maadili ya TFF imekwishakataza, sisi tunafanya nini. Tunakwenda wapi kupata haki yetu. TFF wamekwishakataa. Hapa kuna BMT (Baraza la Michezo la Taifa), je nalo linaweza kusikiliza Rufaa? Hatujui. Kwa hiyo tunajipa hadi Jumatatu, huku tukisubiri hukumu ya Kamati ya Rufaa ya Maadili tujue tunafanya nini,”amesema Wambura. 
    “Sasa tumewaachia wanasheria. Kwa sababu pia tuna katiba ya nchi inayotulinda, kwamba haki zetu tunazipataje, kwa hivyo tunasubiri hadi Jumatatu tupate hiyo hukumu tujue tutakwenda wapi,”amesema..
    Inafahamika FIFA inazuia kesi za mchezi huo kupelekwa kwenye Mahakama za dola na baada ya Wambura kugonga mwamba kwenye mfumo huo haitakuwa ajabu akihamia upande wa pili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAMBURA AJIPANGA KUPAMBANA NA TFF KIVINGINE…ASEMA ATAKULA NAO SAHANI MOJA HADI KIELEWEKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top