• HABARI MPYA

    Friday, March 09, 2018

    YANGA SC YAFUFUA MATUMAINI YA UBINGWA, YAITANDIKA KAGERA SUGAR 3-0…BADO POINTI TATU TU WAIKAMATE SIMBA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imerudi nafasi ya pili baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hiyo ni kutokana na kufikisha pointi 43 baada ya kucheza mechi 20, sasa ikizidiwa pointi tatu tu na vinara, Simba SC.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na Shomari Lawi kutoka Kigoma, aliyesaidiwa na Charles Simon wa Dodoma na Agnes Pantaleo wa Arusha, mabao ya Yanga yalifungwa na Ibrahim Ajib, Yussuph Mhilu na Juma Shemvuni aliyejifunga.
    Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza timu hizo zikimaliza bila kufungana, mvua ya mabao ikaanza kuwamiminikia Kagera Sugar kipindi cha pili.  
    Ibrahim Ajib akinyoosha mikono juu kushangilia baada ya kuifungia Yanga bao la kwanza
    Kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla akiuwahi mpira dhidi ya Thabani Kamusoko wa Yanga
    Emmanuel Martin wa Yanga akimtoka Mwaita Gereza wa Coastal Union
    Ibrahim Ajib akimiliki mpira mble ya Japhet Makalai wa Kagera Sugar
    Pius Buswita wa Yanga akimtoka Juma Shemvuni wa Kagera Sugar

    Alianza mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Ibrahim Ajib dakika ya 53 kufunga kwa penalti baada ya beki Mzanzibari wa Kagera Sugar, Adeymum Saleh Ahmed kuunawa mpira kwenye eneo boksi.
    Akafuatia winga Yussuph Mhilu kufunga la pili dakika ya 75 akimalizia majaro iliyoingizwa kwenye lango la Kagera na kiungo mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa.
    Zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo kumalizika, beki wa Kagera Sugar Juma Shemvuni akamfunga kipa wake, Ramadhani Chalamanda katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na kiungo wa Yanga, Yusuph Mhilu aliyetokea benchi cha pili.
    Katika mchezo wa leo, kiungo Mzimbabwe Thabani Scara Kamusoko alicheza kwa dakika 71 baada ya kukosekana uwanjani tangu Septemba 16, mwaka jana alipoumia kwenye mechi dhidi ya Maji Maji mjini Songea.
    Mabingwa hao wa Tanzania watarudi uwanjani Jumatatu kumenyana na Stand United Uwanja wa Taifa, kabla ya kusafiri kwenda Botswana kwa mchezo wa marudiano na Township Rollers Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, ambako wanatakiwa kushinda 2-0 waingie hatua ya makundi, baada ya kufungwa 2-1 Jumanne Dar es Salaam.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji Mngwali, Said Juma ‘Makapu’, Kelvin Yondani, Pato Ngonyani/Maka Edward dk33, Emmanuel Martin/Juma Mahadhi dk89, Thabani Kamusoko/Mhilu dk71, Pius Buswita, Obrey Chirwa na Ibrahim Ajib..
    Kagera Sugar; Ramadhan Chalamanda, Mwaita Gereza, Adeyun Ahmed/Taita dk59, Juma Shemvumi, Mohamed Fakii, George Kavila, Japhet Makalai/Peter Mwalyanzi dk80, Ally Nassoro ‘Ufudu’, Atupele Green/Omary Daga dk71, Ally Mashaka na Japhary Salum.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAFUFUA MATUMAINI YA UBINGWA, YAITANDIKA KAGERA SUGAR 3-0…BADO POINTI TATU TU WAIKAMATE SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top