• HABARI MPYA

  Jumapili, Mei 28, 2017

  MWILI WA SHOSE ALIYEFARIKI KWENYE AJALI YA MKUDE WAREJESHWA DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWILI wa marehemu Shose Fidelis upo njiani unarejeshwa nyumbani kwao, Dar es Salaam kutoka mkoani Morogoro.
  Shose amefariki dunia mchana wa leo muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali ya mkoa wa Morogoro, kufuatia ajali ya gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 eneo la Dumila mkoani Morogoro.
  Binti huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 na ushei, alikuwa pamoja na Nahodha wa Simba, Jonas Mkude kwenye gari hilo na watu wengine, wakitokea Dodoma, ambako jana timu yao ilitwaa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa ushindi 2-1 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Jamhuri.
  Ndani ya gari hilo walikuwepo pia wapenzi wengine wa Simba, Jasmin na Faudhia ambao wameumia na wamelazwa hospitali ya mkoa wa Morogoro na hali zao ni mbaya.
  Mkude amerejeshwa Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi, wakati dereva ambaye pia ndiye mmiliki wa gari ajulikanaye kwa jina la utani, Rais wa Kibamba yupo chini ya uangalizi wa Polisi.
  Shose Fidelis enzi za uhai wake akiwa na jezi ya SImba na chini akiwa katika picha tatu tofauti ziliozunganishwa
  Katika mchezo wa jana uliodumu kwa dakika 120 baada ya dakika 90 kumalizika timu hizo zikiwa hazijafungana, mabao ya Simba yalifungwa na Frederick Blagnon na Shiza Kichuya kwa penalti, wakati la Mbao lilifungwa na Robert Ndaki.
  Blagnon alianza kuwainua vitini mashabiki wa Simba dakika ya 95 baada ya kumzidi maarifa beki wa Mbao FC kufuatia pasi ndefu ya beki wa kushoto pia, Abdi Banda.
  Lakini Ndaki akaisawazishia Mbao dakika ya 109 akitumia makosa ya Banda aliyezubaa akidhani mfungaji kaotea.
  Wakati wengi wanaamini mchezo utaamuliwa kwa mikwaju ya penalti, lakini refa Ahmed Kikumbo akawazawadia Simba penalti baada ya beki mmoja wa Mbao FC kuunawa mpira uliopigwa na Abdi Banda dakika 119.
  Viongozi wa Simba, Musley Ruwey (kulia) na Hajji Manara wakimjulia hali Fadehil hospitali ya Morogoro
  Wachezaji wa Mbao FC walimzonga refa huyo kabla ya kuamua kutulia na kukubali mchezo uendelee, ndipo winga Shiza Ramadhan Kichuya akaenda kuifungia Simba bao la ushindi na kuamsha shangwe na nderemo Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
  Wakati kikosi cha Simba kimebaki Dodoma kwa ajili ya kwenda kuonyesha Kombe lao Bungeni kesho na baadaye kwenda kucheza mechi ya kirafiki Singida, Mkude na wachezaji wengine wa Simba walioitwa timu ya taifa wamelazimika kuondoka leo kwa usafiri tofauti kurejea Dar es Salaam kujiunga na Taifa Stars.
  Mkude aliomba lifti kwa rafiki yake, Rais wa Kibamba wakati wengine akiwemo beki Abdi Banda walipanda mabasi. Wengine walioitwa Taifa Stars kutoka Simba ni beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, viungo Said Ndemla, Kichuya, Muzamil Yassin, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na mshambuliaji Ibrahim Hajib.     
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MWILI WA SHOSE ALIYEFARIKI KWENYE AJALI YA MKUDE WAREJESHWA DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top