• HABARI MPYA

  Jumatano, Mei 24, 2017

  MBAO WAOMBA REFA ACHEZESHE KWA HAKI JUMAMOSI SIMBA WAKIONE

  Na Mwandishi Wetu, DODOMA
  KOCHA wa Mbao FC, Mrundi Etienne Ndahiragije amewaomba marefa watakaopewa dhamana ya kuchezesha fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) kutenda haki Jumamosi Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
  Mbao watamenyana na vigogo, Simba SC Jumamosi katika fainali kali ya Kombe la ASFC na Mrundi huyo amewaomba marefa kutofanya upendeleo siku hiyo ili apatikane mshindi halali.
  “Sisi kama timu tumekuwa na maandalizi mazuri, na tunajua tunakwenda kucheza na timu kubwa, Simba kama Yanga zote ni timu kubwa sana Tanzania na ukanda huu na tunatarajia ushindani mkubwa,”amesema Ndahiragije.
  Kocha huyo wa zamani wa Vital’O ya kwao, Burundi amesema kwamba kama marefa watachezesha kwa haki mechi hiyo itakuwa nzuri na itakuwa heshima kubwa kwao.
  “Wakichezesha kwa hali itakuwa heshima kubwa kwao na watafanya mechi iwe nzuri sana, sisi tumejiandaa kwa mchezo mzuri na tunatarajia ushindi,”amesema.
  Simba na Mbao zinakutana katika fainali ya Kombe la TFF Jumamosi Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma katika mchezo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
  Hiyo inatokana na viwango vya timu zote katika mechi zao za hivi karibuni kuwa vya kuridhisha na pia matokeo ya mchezo wa mwisho baina yao Aprili 10, Mwanza, Simba ikitoka nyuma kwa 2-0 na kushinda 3-2 ndani ya dakika 10 za mwisho.
  Simba wana kiu kubwa ya kushinda mchezo huo ili kujikatia tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, baada ya kuzidiwa kete na mahasimu wao, Yanga katika Ligi Kuu.
  Lakini Mbao nao wanataka kuweka rekodi, kwanza ya kupanda na kuchukua Kombe hilo na pia kuwa timu ya pili ya Mwanza baada ya Pamba SC kucheza michuanio ya Afrika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MBAO WAOMBA REFA ACHEZESHE KWA HAKI JUMAMOSI SIMBA WAKIONE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top