• HABARI MPYA

  Alhamisi, Mei 25, 2017

  TSHABALALA, NIYONZIMA WACHEZAJI BORA LIGI KUU, MANULA AMBWAGA KASEJA TUZO YA KIPA BORA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  BEKI wa Simba SC, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amefanikiwa kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika sherehe zilizofanyika usiku wa Jumatano ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
  Tshabalala anayecheza upande wa kushoto, baada ya msimu mzuri akiiwezesha Simba kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu nyuma ya mahasimu, Yanga walioibuka mabingwa, amewabwaga 
  Aishi Manula wa Azam, Simon Msuva wa Yanga, Shiza Kichuya wa Simba na Haruna Niyonzima wa Yanga.
  Lakini kiungo wa Rwanda, Niyonzima ‘akainua kwapa’ kwa kunyanyua tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni, akiwashinda beki Mzimbabwe wa Simba, Method Mwanjali na kiungo Mrundi wa Mbao FC, Yusuph Ndikumana.
  Kipa wa zamani wa kimataifa nchini, Steven Nemes (katikati) akimkabidhi Aishi Manula (kulia) tuzo ya Kipa Bora
  Mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Abeid Mziba (kushoto) akishuhudia Mbaraka Yussuf Abeid (katikati) akipokea tuzo yake Mchezaji Bora Chipukizi 
  Simon Msuva akiinua tuzo yake ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu

  Manula naye akainua tuzo ya Kipa Bora akiwashinda Owen Chaina wa Mbeya City na Juma Kaseja wa Kagera Sugar, wakati Msuva amebeba tuzo ya Mfungaji Bora kwa pamoja na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting baada ya wote kufungana kwa mabao 14 kila mmoja.
  Kocha kijana, Mecky Mexime amewashinda makocha wa kigeni, Mcameroon wa Simba, Joseph Omog na Ettiene Ndayiragije wa Mbao FC.
  Mshambuliaji chipukizi wa Kagera Sugar, Mbaraka Yussuf Abeid ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi Kuu akiwaangusha Shaaban Iddi wa Azam FC na Mohammed Issa ‘Banka’ wa Mtibwa Sugar.
  Shaaban Iddi naye akawaangusha mchezaji mwenzake wa Azam, Abdallah Masoud ‘Cabaye’ na 
  Mosses Kitambi wa Simba katika tuzo ya Mchezaji Bora wa U-20, inayojulikana kama tuzo ya Ismail Khalfan wakati Shiza Kichuya akashinda tuzo ya Bao Bora la Msimu alilofunga kwenye mechi dhidi ya Yanga katika ushindi wa 2-1 akiyazidi mabao ya Peter Mwalyanzi wa African Lyon na Zahoro Pazi wa Mbeya. 
  Refa Bora ni Elly Sasii wa Dar es Salaam aliyewashinda Shomari Lawi wa Kigoma na Hance Mabena wa Tanga, wakati Tuzo ya Heshima imekwenda kwa gwiji Kitwana Manara aliyeanza kucheza kama kipa na baadaye mshambuliaji kwa mafanikio makubwa timu ya taifa na klabu ya Yanga na Mwadui FC imeshinda tuzo ya timu yenye Nidhamu.
  Kikosi Bora cha Wachezaji wa Ligi Kuu wa msimu ni; Aishi Manula (Azam), Salum Kimenya (Prisons), Mohammed Hussein (Simba), Yakoub Mohammed (Azam FC), Method Mwanjali (Simba), Kenny Ally (Mbeya City), Simon Msuva (Yanga), Haruna Niyonzima (Yanga), Mbaraka Yusuph (Kagera Sugar), Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting) na Shiza Kichuya (Simba).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TSHABALALA, NIYONZIMA WACHEZAJI BORA LIGI KUU, MANULA AMBWAGA KASEJA TUZO YA KIPA BORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top