• HABARI MPYA

  Jumatatu, Mei 29, 2017

  MKUDE ATEMWA SAFARI YA TAIFA STARS KAMBINI MISRI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NAHODHA Msaidizi wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Jonas Mkude ameenguliwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachoondoka kesho kwenda Misri kwa kambi ya wiki moja.
  Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema kwamba Mkude hatakuwako kwenye msafara huo kutokana na ushauri wa madaktari walioelekeza mchezaji huyo apate mapumziko ya angalau siku nne kuweka akili sawa baada ya ajali aliyopata jana.
  Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga ameridhia na kusema kuwa Mkude ataungana na wenzake Juni 8, mwaka huu timu itakaporejea kutoka Misri. 
  Mkude na watu wengine watano akiwemo dereva, walikuwa kwenye Totota Land Cruiser V8 iliyopinduka hadi porini eneo la Dumila kufuatia tairi kupasuka.
  Jonas Mkude (kushoto) ameondolewa katika kikosi cha Taifa Stras kinachokwenda Misri kesho
  Abiria mmoja, Shose Fidelis alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali ya Mkoa wa Morogoro, wakati wengine, Jasmin na Faudhia wamelazwa hospitalini hapo, huku dereva ambaye pia ndiye mmiliki wa gari ajulikanaye kwa jina la utani, Rais wa Kibamba anashikiliwa na Polisi.
  Mkude alikuwa anatoka Dodoma, ambako juzi aliisaidia Simba kukata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
  Kikosi cha wachezaji 20 wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachodhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti, kinatarajiwa kuondoka kesho Jumanne saa 10.45 jioni kwenda Misri.
  Taifa Stars ambayo itakuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kesho saa 7. 45 mchana inakwenda Misri kufanya kambi ya siku nane kujiandaa na mchezo wa Kundi kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Lesotho Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MKUDE ATEMWA SAFARI YA TAIFA STARS KAMBINI MISRI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top