• HABARI MPYA

    Monday, May 29, 2017

    KUTUMIA ‘VIJEBA’ KWENYE MASHINDANO YA VIJANA NI KUICHIMBIA KABURI SOKA YA AFRIKA

    Na Mahmoud Zubeiry aliyekuwa GABON
    FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 Afrika zilifikia tamati jana kwa Mali kutetea Kombe.
    Historia imewekwa jana jana kwenye michuano hiyo kwa Mali kuwa nchi ya kwanza kutwaa taji la michuano hiyo mara mbili mfululizo, kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Black Starlets ya Ghana Uwanja wa l'Amitie mjini Libreville, Gabon.
    Seme Camara ndiye aliyefunga bao pekee kwa mkwaju wa penalti dakika ya 20 na Mali inaungana na nchi kama Nigeria, Ghana na Gambia zilizotwaa taji hilo mara mbili kila moja tangu mwaka 1995 ilipoanzishwa michuano hiyo.
    Mchezo ulikuwa mkali tangu mwanzo na timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa zamu, lakini washambuliaji pacha wa Mali, Seme Camara na Hadji Drame waliipa wakati mgumu mno safu ya ulinzi ya Ghana.
    Dakika ya 30 Mali walipata penalti nyingine, lakini kipa wa Black Starlets, Danlad Ibrahim akapangua mkwaju wa Mamadou Samake na mwisho wa mchezo, Nahodha wa mabingwa, Mohammed Camara akatajwa Mchezaji Bora wa Mechi.
    Beki wa Mali, Namadi Fofana (kulia) akiwania mpira dhidi ya kiungo wa Ghana, Gabriel Leveh jana
    Mshambuliaji wa Mali, Mamadou Samake akimtoka beki wa Ghana aliyekaa chini
    Wachezaji wa Guinea na Niger wakipambana katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu jana 

    Mabingwa Mali kwa pamoja na washindi wa pili, Ghana, washindi wa tatu Guinea na Niger walioshika nafasi ya nne, wataiwakilisha Afrika kwenye Kombe la Dunia la FIFA la U-17 nchini India mwezi Oktoba.
    Mapema katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, Guinea iliifunga Niger 3-1 na kumalia nyuma ya Ghana.  Mabao ya Guinea yamefungwa na mshambuliaji Djibril Fandje Toure mawili moja kila kipindi na Eldadj Abdourahamane Bah, wakati la Niger lilifungwa na Ibrahim Boubacar Marou.
    Mali iliingia Fainali baada ya kuitoa Guinea kwa penalti 2-0 baada ya sare ya 0-0 mjini Libreville, wakati Ghana nayo iliitoa Niger kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya 0-0 kwenye Nusu Fainali nyingine Uwanja wa Port Gentil. 
    Kwa ujumla, michuano hiyo lishirikisha timu nane kuanzia ngazi ya makundi, Kundi A likiundwa na Gabon, Ghana, Guinea na Cameroon, wakati Kundi B liliundwa na Angola, Niger, Mali na Tanzania iliyokuwa inashiriki kwa mara ya kwanza.
    Serengeti Boys itajilaumu kwa kupoteza nafasi nyingi katika mchezo dhidi ya Angola na kupata ushindi mwembamba wa 2-1 mjini Libreville, kwani baada uya kufungwa 1-0 na Nigeri wakatolewa.
    Tanzania ilianza vizuri tu ikitoa sare ya 0-0 na mabingwa watetezi Mali, lakini katika mchezo wa pili ikashinda 2-1 mbele ya Angola kabla ya kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa mwisho na Niger.
    Tanzania ikafungana kwa pointi na mabao na Niger na mshindi wa pili akapatikana kwa matokeo ya mechi baina ya timu hizo (head to head). Angola ilikuwa timu dhaifu zaidi kwenye Kundi B na ikaaga mikono mitupu. 
    Katika Kundi A, Cameroon ndiyo waliokuwa na matokeo ya kustaajabisha zaidi baada ya kutolewa mapema wakiziacha Ghana na Guinea zikienda Nusu Fanali.
    Wenyeji, Gabon ndiyo waliokuwa na matokeo mabaya zaidi baada ya kupoteza mechi zote tatu. 
    Mali, Ghana, Guinea na Niger zote zimefuzu Fainali za Kombe la Dunia za Oktoba mwaka huu nchini India baada ya kutinga Nusu Fainali tu.
    Wakati michuano hiyo ikihitimishwa jana, tatizo la nchi kuchomekea wachezaji waliozidi umri limeonekana kuendelea kuitafuna soka ya Afrika.
    Karibu timu zote zilizoshiriki mashindano ya mwaka huu Gabon, zilionekana kuwa na wachezaji waliozidi umri unaotakiwa, miaka 17. 
    Timu zimekuwa zikipeleka wachezaji wakubwa ili wazisaidie kufanya vizuri, kuliko vijana wadogo halisi wa chini ya umri wa miaka 17.
    Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeweka kanuni na sheria kali za kupambana na nchi zinazopeleka wachezaji waliozidi umri, lakini bado haijasaidia kukomesha desturi hiyo. 
    Bado CAF ina kazi ya kufanya kuelekea mashindano yajayo ya U-17 nchini Tanzania mwaka 2019 katika kuhakikisha kanuni ya umri inazingatiwa, kwani ni muhimu mno.
    Lengo la kuandaa mashindano ya vijana ni kuandaa wachezaji bora wa baadaye sasa inapotokea nchi zikaleta vijeba wanaharibu dhana nzima ya mashindano yenyewe.
    Na ndiyo matokeo yake katika miaka ya karibuni wachezaji nyota wa Afrika wamekuwa wakipotea baada ya muda mfupi, tofauti na miaka ya nyuma iliposhuhudiwa mchezaji akicheza kwa kiwango cha juu na kuwika kwa zaidi ya miaka 10.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KUTUMIA ‘VIJEBA’ KWENYE MASHINDANO YA VIJANA NI KUICHIMBIA KABURI SOKA YA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top