• HABARI MPYA

  Jumamosi, Mei 27, 2017

  SIMBA KURUDI MICHUANO YA AFRIKA LEO?

  Na Mwandishi Wetu, DODOMA
  SIMBA kurudi michuano ya Afrika leo? Hilo linaweza kuwa swali ambalo wengi wanajiuliza kuelekea fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) Uwanja wa Jamhuri, Dodoma dhidi ya Mbao FC ya Mwanza.
  Simba ilicheza michuano ya Afrika kwa mara ya mwisho, mwaka 2013 na kutolewa na Recreativo de Lobolo ya Angola kwa vipigo vya nyumbani na ugenini, ikifungwa 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na 4-0 ugenini.
  Tangu hapo, Wekundu wa Msimbazi wamekuwa wakizishuhudia Azam na Yanga zikibadilisha ndege kwenda nchi mbalimbali kwa michuano ya Afrika.
  Lakini leo, Simba SC imepata nafasi nzuri ya kukata tiketi ya kurudi kwenye michuano ya Afrika baada ya miaka minne, watakapomenyana na timu ya Mbao iliyopanda Ligi Kuu msimu huu na kuweka rekodi ya kufika fainali ya ASFC.
  Ikitoka kunusurika kushuka Daraja baada ya ushindi wa 1-0 kwenye mechi ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga wiki iliyopita Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza – Mbao FC leo itawania kuwa timu ya pili ya Mwanza kupata tiketi ya kucheza michuano ya Afrika, baada ya Pamba SC.  
  Mchezo wa leo unatarajiwa kuchezeshwa na refa wa Dodoma, Ahmed Kikumbo atakayesaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga na Omary Juma wa Dodoma wakati mwamuzi wa akiba ni Florence Zablon pia wa Dodoma na Kamisaa ni Peter Temu wa Arusha na utaanza Saa 10: 00 jioni na kurushwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam. 
  Bingwa wa Kombe la TFF, lililoachwa wazi na Yanga SC baada ya kutolewa na Mbao FC katika Nusu Fainali kwa kipigo cha 1-0 Mwanza, atajinyakulia kitita cha Sh. Milioni 50 kutoka kwa wadhamini, Azam TV.
  Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana Aprili 10, mwaka huu Simba ilitoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2 ndani ya dakika 10 za mwisho katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. Hiyo ilifanya Simba iwe imeifunga Mbao katika mechi zote za msimu, zu mechi zote zilizozikutanisha timu hizo kihistoria, baada ya Oktoba 20, mwaka jana kushinda pia 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Uwanja wa Taifa.
  Vikosi vya leo vinatarajiwa kuwa; 
  Simba; Agyei Daniel, Janvier Bukungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, James Kotei, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Hajib na Juma Luizio.
  Mbao FC; Benedict Haule, David Mkwasa, Alex Ntiri, Boniface Maganga, Salmin Hoza, Yussuf Ndikumana, Jamal Mwambeleko, George Sangija, Everigustus Bernard, Pius Buswita na Ibrahim Njohole.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA KURUDI MICHUANO YA AFRIKA LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top