• HABARI MPYA

    Friday, February 12, 2016

    YANGA SC BADO 'WANAYACHOMA' UWANJA WA NDEGE DAR, SAFARI YA MAURITIUS SASA...

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    YANGA SC sasa wanatarajiwa kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuania saa 12:30 jioni kwenda mjini, Mauritius kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim. 
    Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kesho Saa 9:30 Alasiri kwa saa za Mauritius Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye Dar es Salaam.
    Awali, Yanga SC ilipanga kuondoka Jumatano wiki hii, lakini ikaahirisha safari baada ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SA), kushindwa kuwapatia ndege ya kuunganisha mapema mjini Johannesburg, kwenda mjini Curepipe.
    Beki Kevin Yondan (kushoto) na kiungo Haruna Niyonzima (kulia) wakiwa kwenye viti vya JNIA jioni hii wakisubiri ndege kwa safari ya Mauritius

    Kwa sababu hiyo, Yanga SC ikaachana na SA na kuamua kukodi ndege ya Shirika la Tanzania (ATC) ambayo walitarajiwa kusafiri nayo Alfajiri ya leo, lakini hadi sasa wachezaji wameganda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
    Taarifa za sasa zinasema msafara wa Yanga SC umehakikishiwa kuwa umekwisharuka hadi kufika Saa 12:30 jioni kwa safari ya saa nne angani hadi Maurtius, maana yake watafika kuanzia Saa 6:30 usiku.
    Sababu za kuchelewa ni ndege waliyotarajiwa kusafiri nayo kupata dosari na kulazimika kufanyiwa marekebisho kutwa nzima.
    Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ameamua kubeba kikosi chake chote kwa safari ya Mauritius, kwani baada ya mchezo huo Jumamosi, ndege hiyo ya ATC itaichukua timu hiyo kuipeleka Pemba, visiwani Zanzibar.
    Yanga SC itaweka kambi kisiwani Pemba, kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya mahasimu Simba SC, Februari 20, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC BADO 'WANAYACHOMA' UWANJA WA NDEGE DAR, SAFARI YA MAURITIUS SASA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top