• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 24, 2016

  AISHI ALIFANYA KOSA LA KIMCHEZO, LAKINI KESSY, BANDA…

  KOCHA Mganda, Jackson Mayanja amelazimika kuanza kumtetea beki wake, Hassan Ramadhani Kessy mbele ya mashabiki wa Simba SC walioanza kupoteza imani naye.
  Hiyo inafuatia Simba SC kufungwa mabao 2-0 watani wao, Yanga SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuporomoka hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 
  Matokeo hayo yanaifanya Yanga ifikishe pointi 46 baada ya kucheza mechi 19 na kurejea kileleni, wakati Simba SC iliyocheza mechi 20, inabaki na pointi zake 45 na kushuka hadi nafasi ya tatu, huku Azam FC yenye pointi 45 pia inapanda nafasi ya pili kwa wastani mzuri wa mabao.

  Kipigo hicho kimewaumiza wana Simba kutokana na kwamba ni cha pili mfululizo katika msimu mmoja, kutoka kwa watani wao hao, baada ya Septemba 26, mwaka jana kufungwa pia 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
  Simba SC haijawahi kufungwa mechi zote za msimu za Ligi Kuu na watani wao hao tangu mwaka 1999 – na ndiyo maana matokeo hayo yamewaumiza mno Wekundu wa Msimbazi.
  Na baada ya mchezo, mashabiki na wapenzi wa Simba SC wamekuwa wakiwatupia lawama mabeki, Hassan Kessy na Abdi Banda kwamba walichangia timu kupoteza mechi hiyo muhimu kwao katika harakati za kuwania taji la kwanza la ubingwa wa Ligi Kuu tangu mwaka 2011.
  Banda alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 24 tu ya mchezo, baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na refa Jonesia Rukyaa wa Kagera kwa kumchezea rafu mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma – dakika tatu baada ya kuonyeshwa kadi ya kwanza ya njano kwa kumchezea rafu mchezaji huyo huyo wa Zimbabwe.
  Kessy akamrudishia pasi fupi kipa Vincent Angban ambayo ilinaswa na Ngoma aliyemzunguka kipa wa Ivory Coast na kuifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya 39.
  Kocha Mganda wa Simba, Jackson Mayanja alisema baada ya mechi kwamba kutolewa kwa Banda mapema kulitibua mipango yake hata wakapoteza mchezo na akasikitikia makosa yaliyowapa bao rahisi wapinzani kipindi cha kwanza.
  Kocha yeyote angesema hivyo baada ya mchezo, kwa sababu ndiyo hali halisi – kwamba Banda aliigharimu timu kwa kutolewa kwa kadi nyekundu na makosa ya Kessy ndiyo yaliipa bao la kwanza rahisi Yanga.
  Lakini wakati yote haya yakiendelea, Simba, wanapaswa kukumbuka kwamba mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, hivyo wanapaswa kuwasamehe wachezaji wao na kushikamana kama timu kuelekeza nguvu zao katika mechi zijazo.
  Haitakuwa vyema thamani ya Banda na Kessy ikaporomoka mara na ghafla kwenye timu – tu kwa sababu ya dhana zisizo za ukweli kama ilivyo kawaida timu hizo kongwe (Simba na Yanga) zinapopoteza mechi hutafuta sababu hata za nje ya Uwanja ili kuwabebesha mzigo wa lawama wachezaji. 
  Februari 14, mwaka huu, kipa Aishi Manula alifanya kosa ambalo huwezi kuamini kipa wa timu ya taifa anaweza kufanya – ambalo liliigharimu Azam FC kupoteza mchezo wa Ligi mbele ya wenyeji Coastal Union kwa kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Aishi alidaka mpira na kuanguka chini kabla ya kuanza kuugulia maumivu, lakini kisheria alipaswa kuutoa nje mpira au kupiga yowe na kunyoosha mkono ili refa amuone na kusimamisha mchezo – badala yake aliulalia tu mpira kwa sekunde kadhaa hadi mwamuzi alipopiga filimbi na kuamuru pigo la adhabu lielekezwe Azam FC.
  Beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Miraj Adam, mtaalamu wa kupiga mipira ya adhabu akaenda kuifungia bao pekee Coastal Union.
  Kwa Azam FC yalichukuliwa kama makosa ya kawaida mchezoni na labda Aishi, kipa chipukizi mwenye kipaji kizuri alipata fundisho zuri katika maisha yake ya ulinda mlango.
  Aishi akasimama tena langoni katika mchezo uliofuata wa Ligi Kuu wa Azam FC na kuiongoza timu yake kushinda mabao 3-0 ugenini dhidi ya Mbeya City Jumamosi– huo ndiyo uanamichezo tunaoutarajia kuuona hata kwa Simba SC juu ya Kessy na Banda baada ya makosa yao mwishoni mwa wiki.
  Narudia kuwaambia Simba, kwamba; mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, huvyo wanapaswa kuwasamehe wachezaji hao, kama ambavyo Azam wamefanya kwa Aishi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AISHI ALIFANYA KOSA LA KIMCHEZO, LAKINI KESSY, BANDA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top