• HABARI MPYA

    Saturday, February 20, 2016

    NI MAZEMBE AU ETOILE KUBEBA SUPER CUP YA CAF LEO?

    MABINGWA wa Afrika, TP Mazembe wakichagizwa na mafanikio ya nchi yao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutwaa Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) nchini Rwanda, leo watawania taji la Super Cup la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
    Mapema mwezi huu, DRC ilitwaa Kombe la CHAN, michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee kwa mara ya pili tangu ianzishwe mwaka 2009, walipoilaza  Mali mabao 3-0 kwenye fainali Rwanda.
    Nyota kadhaa wa Mazembe, akiwemo Nahodha, Joel Kimwaki na mshambuliaji Jonathan Bolingi walikuwemo kwenye kikosi cha CHAN ambacho baada ya ushindi huo walizawadiwa gari aina ya Prado na rais Joseph Kabila.

    Mabingwa hao mara tano Afrika watapigania taji la tatu la Super Cup leo Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, baada ya awali kulitwaa katika miaka ya 2010 na 2011.
    Lakini 'The Ravens', wataikosa huduma ya kinara wao mabao, Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta, aliyejiunga na KRC Genk ya Ubelgiji Januari baada ya miaka minne ya kuwa na klabu hiyo ya Kongo.
    'Samagoal' aliondoka Mazembe akiiachia Kombe la Ligi ya Mabingwa huku akiibuka mfungaji bora na kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
    Kocha Patrice Carteron pia ameondoka baada ya msimu mzuri, nafasi yake ikichukuliwa na Mfaransa mwenzake, Hubert Velud, ambaye umaarufu wake aliupatia Algeria na alipokuwa kocha wa Togo.
    Lakini mshambuliaji mwingine, Mtanzania Thomas 'Rambo' Ulimwengu bado yupo Mazembe na leo anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo,
    Mazembe wataingia kwenye mchezo wa leo wakitoka kutoa sare ya bila mabao na St Eloi Lupopo Jumatano katkka Ligi Kuu ya DRC.
    Ikumbukwe, Etoile du Sahel mabingwa wa Kombe la Shirikisho, pia wametwaa mara mbili taji Super Cup la CAF mwaka 1998 na 2008, wakati mwaka 2004 na 2007 walikuwa wa pili.
    ES Setif ya Algeria ndiyo walitwaa Super Cup mwaka jana baada ya kuifunga Al Ahly ya Misri kwa penalti 6-5 baada ya sare ya 1-1 mjini Blida.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI MAZEMBE AU ETOILE KUBEBA SUPER CUP YA CAF LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top