• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 25, 2016

  ULIMWENGU: NI MAPEMA KULIONA PENGO LA SAMATTA MAZEMBE

  Thomas Ulimwengu akiwa na Medali ya Dhahabu na taji la Super Cup ya CAF Jumamosi kwenye chumba cha kubadilishia nguo mjini Lubumbashi baada ya kuifunga Etoile du Sahel 2-1
  Na Mwandishi Wetu, LUBUMBASHI
  KWA kijana yeyote anayechipukia kisoka Afrika, kucheza Ulaya ndiyo ndoto kuu, kwa sababu siyo tu ya maslahi bali kufuata Ligi zenye mvuto zaidi na zinazokutanisha wachezaji kutoka pembe tofauti za dunia.
  Lakini katika hatua za mwanzo, mchezaji anapoanza kupata mafanikio makubwa akiwa ndani ya ardhi ya Afrika ni faraja kubwa.
  Mwishoni mwa wiki, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu aliweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kushinda taji la Super Cup ya CAF.
  Hiyo inafuatia timu yake, Tout Puissant Mazembe kuifunga Etoile du Sahel ya Tunisia mabao 2-1 Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi.
  Sasa katika kabati lake, Ulimwengu ana Medali za dhahabu za Ligi ya Mabingwa Afrika na Super Cup pamoja na Medali ya Fedha ya Kombe la Shirikisho Afrika.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE ilifanya mahojiano na Ulimwengu baada ya mafanikio ya Jumamosi, mchezo ambao aliingia kutokea benchi kipindi cha pili, endelea.
  Thomas Ulimwengu amekuwa Mtanzania wa kwanza kushinda Super Cup ya CAF

  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Habari za leo Thomas.
  ULIMWENGU: Nzuri tu kaka
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Hongera sana kwa ushindi huu ws kihistoria kwako, kwa klabu na kwa nchi zote, Tanzania na DRC.
  ULIMWENGU: Asante sana kaka.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Vipi unajisikiaje baada ya ushindi huu.
  ULIMWENGU: Najisikia furaha sanaa, maana siyo jambo dogo kabisa hilo.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Hadi sasa umefikisha mataji mangapi jumla uliyotwaa na Mazembe.
  ULIMWENGU: Kama nane hivi, Ligi Kuu (DRC) tumechukua mara tatu katika misimu minne niliyocheza hapa. Ligi ya Mabingwa moja, Super Cup ya CAF moja na makombe mengine mengine madogo ya hapa, kuna Super Cup ya DRC mara tatu.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Hongera sana, (Jumamosi) ulianzia benchi dhidi ya Etoile na wakati wa kocha aliyeondoka (Mfaransa Patrice Carteron) ulikuwa unaanza kikosi cha kwanza. Unadhani kwa nini Mfaransa Hubert Velud alikuanzishia kwenye kiti kirefu?
  ULIMWENGU: Hapana, ni mechi ile tu maana mechi zote zilizopita nilikua nacheza na maumivu ya mguu na nilijiumiza tena kwenye mechi dhidi ya FC Lupopo (0-0 wiki iliyopita), hivyo nilikua mtu mwenye maumivu mguuni. Hapa sasa ninajiandaa kwenda kwa daktari.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Sawa, Machi 13 mnaanza Ligi ya Mabingwa. Unadhani utakuwa fiti kabisa?
  ULIMWENGU: Hapo nitakuwa fiti, muda mrefu sanaa kufanya matibabu na kuwa fiti.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Kulingana na ulivyoiona mechi na Etoile na ukirejea mechi za Ligi ya Mabingwa, unadhani pengo la (Mbwana) Samatta lipo Mazembe?
  ULIMWENGU: Kwa mechi kama hizi huwezi kuona umuhimu wa mtu aliyetoka, subiri tuanze mechi kubwa, kisha ndiyo tutaona umuhimu wake.
  Thomas Ulimwengu akiichezea Tanzania dhidi ya Algeria mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 

  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Unaelekea kumaliza mkataba wako mwishoni mwa msimu, je mustakabali wako ukoje?
  ULIMWENGU: Mambo yangu kama hayo nitasema pale nitakapoyakamilisha, ila malengo yangu ni kuondoka Mazembe.
  [BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Unadhani Mazembe itakuruhusu kuondoka?
  ULIMWENGU: Kama nitakuwa nimemaliza Mkataba, watanizuiaje?
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Utamaliza Mkataba Aprili mwishoni wakati Mazembe ipo kwenye mashindano ya msimu kama Ligi ya Mabingwa na Ligi ya DRC, wakati huo huo dirisha la usajili litafunguliwa Agosti. Hapo itakuwaje?
  ULIMWENGU: Ni kweli, hilo hata mimi nalijua, nadhani kwanza tusubiri nimalize Mkataba na Mungu anijaalie kupata mwingine sehemu nyingine, mengine yatafuata. Kama kubaki Mazembe kwa makubaliano maalum kumalizia msimu au vipi.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Unaizungumziaje soka katika maisha yako.
  ULIMWENGU: Mpira ndiyo maisha yangu kwa sasa, nauheshimu ndiyo maana nipo hapa nilipo na nimepata mengi sanaa kupitia kazi yangu.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Baadhi ya uliyovuna kutokana na mpira?
  ULIMWENGU: Vitu ambavyo vinamkamilisha binadamu mwenye maisha mazuri vyote nimepata.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Si kujivuna, bali kuwaonyesha chipukizi umuhimu wa bidii, uvumilivu na kujitoa...tuambie nyumba za aina gani na wapi mashamba labda kama yapo na magari mangapi na ya aina gani.
  ULIMWENGU: Huwa sipendi kuweka hayo maisha kwenye vyombo vya habari.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Wazazi wanayapokeaje mafanikio yako?
  ULIMWENGU: Kwa kweli nawashukuru sana wazazi wangu, Mzee Emmanuel Ulimwengu na mama (Justina Ulimwengu) kwa kuwa nyuma ya harakati zangu wakati wote. Na sasa wanafurahia sana matunda haya.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Ulienda Mazembe ukitokea Sweden, kabla ulienda Ujerumani ukitokea Moro United iliyokutoa Taasisi ya Soka Tanzania (TSA), hebu tupe hii historia na sababu za kupitia Ulaya kuingia Mazembe.
  ULIMWENGU: Sweden nilikwenda kwenye akademi, baadaye nikapata timu Ujerumani, lakini ikashindikana kupata kibali cha kucheza, ndiyo nikaja Mazembe.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Ni kijana kamili sasa, vipi una mchumba au mke?
  ULIMWENGU: Nina mchumba tu.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Mipango ya ndoa?
  ULIMWENGU: Ipo, wakati ukifika nitakuletea kadi ya mchango kaka…hee heee
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Wakati unafurahia mataji ya klabu, ukirudi kwenye timu ya taifa hali ni tofauti, unasemaje?
  Thomas Ulimwengu akiichezea Tanzania dhidi ya Nigeria mechi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika

  ULIMWENGU: Dah! Hapo kichwa kinauma ndugu yangu. Soka ya Tanzania ina matatizo mengi sana, ni ngumu kuweza kuyatatua kwa wakati mmoja, inahitaji muda na pia kupata viongozi watakaoweza kusimamia mageuzi katika soka yetu. Ila kwa kuanzia si vibaya kama vijana wengi tukapata nafasi za kucheza Ulaya, ili baadaye tuje kuisaidia timu yetu ya taifa.
  Wachezaji wa Tanzania wana vipaji sana, ila wana mapungufu madogo tu na inahitaji watu kupata nafasi kama ambayo mimi na Mbwana (Samatta) tulipata. Kucheza klabu kama Mazembe ambayo inacheza mashindano mengi makubwa na ipo kwenye ligi yenye ushindani mkubwa, ambao unasaidia kukuza uwezo wa mchezaji.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Wakati huo huo mpo kwenye mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika, mmefungwa na Misri ugenini, mmetoa sare na Nigeria nyumbani, mna nafasi gani sasa?
  ULIMWENGU: Nafasi bado tunayo, ila ni ndogo. Tunatakiwa kushinda mechi zote zilizobaki kisha tuangalie kundi likoje. Naomba nikuombe samahani ndugu yangu, natakiwa kujiandaa kwenda kumuona Daktari.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Hapana shaka Thom, nashukuru kwa ushirikiano wako.
  ULIMWENGU: Asante sana, tuko pamoja.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Asante. Siku njema na ninakutakia upone haraka na urejee kikamilifu uwanjani.
  ULIMWENGU: Amin, asante kaka yangu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ULIMWENGU: NI MAPEMA KULIONA PENGO LA SAMATTA MAZEMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top