• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 21, 2016

  PLUIJM: PATO NGONYANI ALISAIDIA SANA VITA YA KUCHINJA MNYAMA JANA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amesema kwamba kumtumia beki Pato Ngonyani kama kiungo wa ulinzi ndiko kulimsaidia jana kuwafunga Simba SC.
  Akizungumza baada ya mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ambao Yanga ilishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Mholanzi huyo alisema alisema kubadili mfumo na kuchezesha viungo watatu kulimsaidia kuwadhibiti Simba katika eneo la katikati ya uwanja.
  Pluijm alimwagia sifa chipukizi Ngonyani kwamba kucheza vizuri kama kiungo wa ulinzi, akifuata vyema maelekezo aliyopewa.
  Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema Pato Ngonyani alisaidia vita ya kuua mnyama jana 

  “Tulijua Simba wana viungo wazuri na sisi tukaweka viungo watatu katikati, ili kuwe na uwiano sawa na tulifanikiwa kwa hilo” alisema Pluijm.
  “Pato bado ana umri mdogo, akiendelea kujituma na nidhamu, naona atakuja kuwa mchezaji mzuri siku za baadaye” alisema kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana.
  Yanga SC jana ilirejea kileleni mwa Ligi Kuu baada ya kuwachapa 2-0 watani wao, Simba SC, mabao ya Donald Dombo Ngoma kipindi cha kwanza na Amissi Joselyn Tambwe kipindi cha pili.
  Yanga sasa inafikisha pointi 46 baada ya kucheza mechi 19, wakati Simba SC iliyocheza mechi ya 20 leo, inabaki na pointi zake 45 na kushuka hadi nafasi ya tatu.
  Matokeo hayo yanaifanya Yanga SC ivune pointi sita msimu huu kwa watani, baada ya mechi ya mzunguko wa kwanza pia kushinda 2-0 Septemba 26, mwaka jana mabao ya Tambwe kipindi cha kwanza Malimi Busungu kipindi cha pili.
  Hii ni mara ya kwanza Yanga inaifunga Simba SC mechi zote za msimu za Ligi Kuu tangu mwaka 1999, msimu ambao Mtibwa Sugar waliibuka mabingwa.
  Msimu wa 1999, wakati huo Ligi Kuu inadhaminiwa na bia ya Safari Lager inayotengenezwa na kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Yanga iliichapa Simba 3-1 Mei 1, 1999 mabao ya Idd Moshi, Kali Ongala na Salvatory Edward la wapinzani likifungwa na Juma Amir Maftah, wakati marudiano wana Jangwani wakashinda 2-0 Agosti 29, 1999 mabao ya Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ na Mohamed Hussein 'Mmachinga'.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PLUIJM: PATO NGONYANI ALISAIDIA SANA VITA YA KUCHINJA MNYAMA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top