• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 22, 2016

  KENYA YAPATA KOCHA MPYA MZALENDO BAADA YA MZUNGU KUONDOKA

  TIMU ya taifa ya Kenya, Harambee Stars sasa itakuwa chini ya Stanley Okumbi anayechukua nafasi ya Mscotland, Bobby Williamson aliyeondoka.
  Sasa kocha huyo wa zamani wa timu za vijana za Kenya ataiongoza Harambee Stars katika mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
  Mwenyekiti mpya wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Nick Mwendwa amesema mwishoini mwa wiki kwamba, Okumbi, aliyeifundisha timu ya Ligi Kuu ya nchi hiyo, Mathare United msimu uliopita, atakuwa kocha wa muda wa Harambee Stars itakapomenyana na Guinea Bissau ugenini mjini Bissau mwezi ujao.

  Stanley Okumbi ndiye kocha mpya wa Harambee Stars baada ya kuondoka kwa Mscotland Bobby Williamson

  Williamson, ambaye amekuwa kocha wa Kenya tangu Agosti mwaka 2014, inaaminika anadai malimbikizo ya mishahara kiasi cha dola za Kimarekani 30,000 chini ya uongozi uliopita wa FKF wa Sammy Nyamweya, ambaye aliangushwa katika uchaguzi wa mwezi uliopita.
  Kiungo wa zamani wa kimataifa wa Kenya, Musa Otieno, aliyekuwa Msaidizi wa Williamson ataendelea kuwa Kocha Msaidizi Harambee Stars chini ya Okumbi.
  Chini ya Williamson, Kenya ilisuasua katika mechi zake mbili za kwanza kuwania tiketi ya AFCON mwakani baada ya kutoa sare ya 1-1 na Kongo na kufungwa 2-1 nyumbani na Zambia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KENYA YAPATA KOCHA MPYA MZALENDO BAADA YA MZUNGU KUONDOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top