• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 28, 2016

  TUNAVYOCHUKULIA CHAD SIVYO, LABDA TUMEWASAHAU TU!

  TANZANIA ilianza vibaya katika mechi za Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani, baada ya kuambulia pointi moja katika mechi mbili.
  Taifa Stars ilianza kwa kufungwa mabao 3-0 nchini Misri na Mafarao Uwanja wa Borg el Arab Juni 14, mwaka jana mabao ya Rami Rabia dakika ya 61, Basem Morsi dakika ya 65 na Mohamed Salah dakika ya 70.
  Baada ya mchezo huo, Taifa Stars iliyofungwa pia 3-0 nyumbani na Uganda katika mchezo wa kufuzu CHAN ya mwaka huu, ilimfukuza kocha Mholanzi, Mart Nooij na mzalendo Charles Boniface Mkwasa akachukua nafasi.

  Mchezo wa pili, Taifa Stars ikalazimishwa sare ya 0-0 na Nigeria nyumbani Septemba 5 mwaka jana kabla ya kwenda kutolewa katika mechi ya mchujo wa kufuzu Kombe la Dunia baada ya kufungwa jumla ya mabao 9-2 na Algeria. 
  Machi 25 mwaka huu, Taifa Stars itasafiri hadi Chad kumenyana na wenyeji, Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya mjini N'Djamena katika mchezo wa Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2017 nchini Afrika Kusini.
  Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Machi 28, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na huo utakuwa mchezo wa nne kwa Taifa Stars katika kundi hilo, baada ya kufungwa ugenini 3-0 na Misri na kulazimishwa sare ya 0-0 na Nigeria Dar es Salaam.
  Taifa Stars itacheza nyumbani na Misri kabla ya kusafiri kwenda Nigeria kwa mchezo wa mwisho wa kundi hilo, kisha kuangalia mustakabali wake wa kufuzu.
  Ikumbukwe kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za Mataifa ya Afrika mwaka 1980, ambako iliishia hatua ya makundi baada ya kufungwa 3-0 na wenyeji, 2-1 na Misri na sare ya 1-1 Ivory Coast. Maana yake Watanzania tuna kiu ya kuiona tena timu yetu ya taifa ikicheza mashindano hayo makubwa.
  Lakini wakati michezo miwili muhimu dhidi ya Chad inakaribia, ambayo Stars ikishinda inaweza kabisa kufufua matumaini ya kufuzu AFCON ya mwakani, hadi sasa si kocha wa timu ya taifa, Charles Boniface Mkwasa au kiongozi yeyote wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) aliyejitokeza kuongelea mikakati japo ya maandalizi.
  Tatizo letu moja kubwa Watanzania ni dharau – hapa inaanza kujitokeza picha kama ya kuwadharau Chad na kuona kwamba mechi zilizopo mbele si ngumu.
  Mchezo ufuatao ungekuwa dhidi ya Misri au Nigeria tungesikia pilika za wakubwa za maandalizi na kuunda Kamati, lakini kwa Chad tunasubiri wiki ya mwisho timu iingie kambini.
  Lakini kumbe baada ya kushindwa kupata matokeo mazuri katika mechi ngumu, sasa tunapaswa kuwekeza maandalizi mazuri katika mechi ambazo tunaamini ni nyepesi kidogo, ili tuwe vizuri na kushinda.
  Ukweli ni kwamba Taifa Stars haiwi timu ya kucheza vyema siku zote bila maandalizi mazuri na ya muda mrefu kidogo na hilo tumeliona katika michezo yetu iliyopita, kwamba wachezaji wanapopata kambi ya pamoja japo wiki mbili au zaidi, ndiyo hucheza vizuri.
  Ukiitazama timu yetu ya taifa kwa sasa, zaidi ya Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jumhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Mrisho Ngassa wa Free State Stars ya Afrika Kusini hatuna mchezaji mwingine wa kujivunia.
  Wapinzani wetu, Chan wana wachezaji wengi tishio kama Ezechiel N'Douassel wa Sfaxien ya Tunisia, Rodrigue Ninga wa Montpellier ya Ufaransa, Marius Mbaiam wa Belfort ya Ufaransa, Leger Djime anayechezea klabu ya nyumbani kwa sasa, Foullah Edifice baada ya kuchezea Al Nasr ya Misri na Difaa El Jadida ya Morocco, Mahamat Labbo wa R.O.C. de Charleroi-Marchiennena ya Ubelgiji na Karl Max Barthelemy wa  Difaa El Jadidi  ya Morocco.
  Tunaidharau Chad ambayo mwaka 2014 tulikutana nayo katika mchujo wa kufuzu Kombe la Dunia Raundi ya kwnza na kuitoa kwa mbinde. 
  Walitufunga 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na sisi tukawafunga 2-1 kwao mjini N'Djamena, hivyo tukafuzu kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya sare ya jumla 2-2. 
  Safari hii hatukutani nao kwenye mtoano tena, bali ni mechi za makundi tunazohitaji kuvuna pointi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu AFCON.
  Lakini kwa mzaha ambao unaendelea hadi sasa, sioni dalili za Taifa Stars kuchanua mbele ya Chad, timu ambayo inachukuliwa kama nyepesi zaidi katika kundi letu, wakati pia tuna michezo migumu dhidi ya Misri na Nigeria.
  Tunavyoichukulia Chad sivyo. Tunajidanganya, inaweza kuwa timu nzuri kuliko Taifa Stars yetu na tunachopaswa kwa sasa ni kuamka usingizini na kuanza mkakati wa maandalizi, utakaofuatiwa na maandalizi mara moja. Wikiendi njema. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TUNAVYOCHUKULIA CHAD SIVYO, LABDA TUMEWASAHAU TU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top