• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 25, 2016

  WACHEZAJI WA COASTAL UNION WAGOMA HAWAJALIPWA MISHAHARA MIEZI MITATU

  Na Mwandishi Wetu, TANGA
  WACHEZAJI wa Coastal Union ya Tanga wamegoma ili kushinikiza kulipwa malimbikizo ya mishahara yao ya miezi mitatu.
  Kundi la wachezaji lilifika makao makuu ya klabu, barabara ya 13 mapema asubuhi ya leo mjini Tanga wakiwa na mabango yenye kuwasilisha kilio chao cha kudai mishahara.
  Na wachezaji hao hawakwenda kufanya mazoezi leo asubuhi  – huku ikiwa haijulikani msimamo wao huo utaendelea kwa muda gani. 
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Coastal Union, Oscar Assenga ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kwamba amesikia taarifa hizo, lakini hazijui vyema kwa sababu yupo nje ya Tanga.
  Wachezaji wa Coastal Union wakiwa na bango lao makao makuu ya klabu leo

  “Mimi sipo Tanga mjini, ila nimezisikia sikia hizo taarifa juu juu tu, ninachofanya kwa sasa ni kuwasiliana na uongozi wa juu wa Coastal ndipo nitakuwa katika nafasi ya kulizungumzia hilo,”amesema Assenga.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu kwamba hali ya kiuchumi ndani ya Coastal Union si njema kwa sasa kufuatia kuondoka kwa mdhamini, kampuni y Pembe Desemba mwaka jana.
  Na hali imezidi kuwa mbaya ndani ya Coastal kuanzia Januari na kwa kiasi kikubwa hiyo ndiyo inachangia hata mwenendo mbaya wa timu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa sababu wachezaji hawana morali.
  Coastal Union inashika nafasi ya 14 kwenye Ligi Kuu yenye timu 16, ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi 20.
  Na mabingwa hao wa mwaka 1988, wanawazidi kwa wastani wa mabao tu ndugu zao, African Sports walio nafasi ya 15 wakiwa na pointi 16 pia, baada ya kucheza mechi 20, wakati JKT Ruvu yenye pointi 15 za mechi 20 ndiyo inashika mkia.
  Kwa ujumla hali imekuwa si nzuri Coastal Union tangu mwaka juzi alipoondoka aliyekuwa mfadhili mkuu wa timu hiyo, Nassor Bin Slum, ambaye pia ni mpenzi na mwanachana.
  Bin Slum aliyekuwa anaisadia kwa hali na mali Coastal, aliondokana baada ya kutofautiana na uongozi chini ya Mwenyekiti wa wakati huo, Ally Aurora. 
  Mwenyekiti wa sasa wa Coastal Union, Dk Ahmed Twaha amesema kwamba watakutana na wachezaji leo jioni na baada ya hapo watatoa taarifa ya mustakabali wa tatizo hilo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WACHEZAJI WA COASTAL UNION WAGOMA HAWAJALIPWA MISHAHARA MIEZI MITATU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top