• HABARI MPYA

    Friday, February 26, 2016

    NDANDA, COASTAL WATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA TFF

    Na Waandishi Wetu, MTWARA NA TANGA
    TIMU za Coastal Union ya Tanga na Ndanda FC ya Mtwara zimekwenda Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup kufuatia ushindi wa nyumbani leo.
    Coastal Union imeifunga 1-0 Mtibwa Sugar ya Morogoro Uwanja wa Mkwakwani, Tanga bao pekee la Adeyoum Saleh Ahmed dakika ya 14 baada ya krosi ya beki Miraj Adam.
    Ndanda imeifunga JKT Ruvu ya Pwani mabao 3-0 Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
    Ndanda ambao mchezo wao wa kwanza katika michuano hiyo ambayo bingwa wake atawakilisha Taifa katika Kombe la Shirikisho barani Afrika, waliichapa Mshikamano kwa jumla yamagoli 5-0 leo hii wamelipa kisasi cha kuchapwa magoli 3-1 na Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliochezwa katika uwanja huo katika mzunguko wakwanza.

    Mchezo huo ulionekana kupooza katika dakika za mwanzoni kwa timu zote kucheza kwa tahadhari kubwa kuhofia kuruhusu goli la mapema na kufanikiwa kumaliza dakika 20 za mwazo zikiwa hazijafungana.
    Kadri muda ulivozidi kwenda mchezo ulionekana kuchangamka huku Ndanda wakipanga mashambulizi zaidi langoni mwa Ruvu ambapo katika dakika ya 27 mchezaji Omari Mponda alifanikiwa kuipatia goli la kuongoza Ndanda baada ya kutumia vyema mpira wa kona iliyopigwa na Paul Ngalema na kushindwa kuokolewa na walinzi wa Ruvu.
    Zikiwa zimesalia dakika 4 kabla ya timu hizo kwenda mapumziko, mlinzi wa pembeni upande wa kushoto wa Ndanda Fc, Paul Ngalema ambaye leo alionekana kuwa na madhara zaidi kufuatia krosi zake alizokua akizielekeza langoni mwa Ruvu, aliipatia timu yake bao la pili kwa kuachia shuti lililomshinda mlinda mlango wa Ruvu Shaban Dihile, hivyo hadi timu zinakwenda mapumziko ni Ndanda ambao walikuwa mbele kwa magoli hayo mawili.
    Ruvu wanaonolewa na Kibaden Mputa, walirudi kipindi cha pili wakiwa na dhamira ya kutaka kurejesha magoli hayo lakini waliduwaa baada ya Atupele Green kutumia dakika Tatu tu baada ya kuanza kipindi cha pili kuweza kuandika goli la Tatu kwa kuachia shuti kali kwa guu la kushoto na kuitimisha karamu hiyo ya magoli katika mchezo huo.
    Ndanda waliwabadilisha Omega Seme, Omary Mponda na Kasian Ponera alaiyeumia na nafasi zao kuzibwa na Jackson Mkwera, Salum Minelly na Masoud Ally huku Ruvu wakimbadilisha George Minja aliyeumia na kumuingiza Cecil Efrem.
    Kadi ya njano ilitoka moja katika mchezo huo ikielekezwa kwa mlinzi wa Ndanda, Salvatory Ntebe baada ya kujibizana na mwamuzi.
    Mchezaji Saady Kipanga wa Ruvu alikiri kuwa walicheza vibaya na kutoa mwanya kwa wapinzani wao kuweza kutumia makosa yao na kupata magoli huku akiwasihi mashabiki wao kutokata tama kutokana na mwenendo wao mbaya katika ligi unaopelekea kushika mkia.
    Kocha wa Ruvu, Kibaden Mputa hakusita kukiri kuzidiwa na wapinzani wake na kudai kuwa safu yake ya ulinzi haikucheza vizuri kiasi cha kuruhusu idadi hiyo ya magoli ambapo wakati wanaelekea katika mchezo hawakutegemea kutokana na kuwa na kumbukumbu ya kuwafunga awali.
    Naye kocha msaidizi wa Ndanda, Mussa Mbaya, aliendelea kutamba na kukisifu kikosi chake kucheza kwa uelewano nzuri na kuahidi kuzidi kuwafurahisha mashabiki wao hasa katika michezo ya ligi kuu iliyosalia huku wakielekeza nguvu katika mchezo wao ujao dhidi ya Toto Africans utakaochezwa jijini Mwanza wiki ijayo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NDANDA, COASTAL WATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top