• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 29, 2016

  SIMBA SC YAANZA MAZUNGUMZO YA MKATABA MPYA NA KESSY

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba imechukua maamuzi mazito dhidi ya beki wake chipukizi wa kulia, Hassan Ramadhani Kessy ambaye kwa sasa mashabiki wa timu hiyo wanamuangalia kwa hasira.
  Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE kwamba wameanza mchakato wa kumuongezea Mkataba Kessy, wakati huu wa sasa unaelekea kufikia tamati mwishoni mwa msimu.
  Aveva amesema kwamba mazungumzo ya Mkataba mpya wa Kessy awali yalikwamishwa na Meneja wa mchezaji huyo, Athumani Tippo ‘Zizzou’ ambaye alitaka yafanyike baada ya msimu.
  Hassan Ramadhani Kessy kushoto yupo kwenye majadiliano ya Mkataba mpya na Simba SC

  “Lakini imebidi tulazimishe yafanyike, ili matokeo yoyote ya mchezoni yasije yakaathiri hili baadaye,”alisema Aveva. 
  Rais huyo akatolea mfano kosa lililofanywa na Kessy katika mchezo dhidi ya mahasimu, Yanga SC Jumamosi wiki iliyopita kwamba ‘limemharibia’ kidogo mchezaji huyo mbele ya wapenzi wa Simba.
  “Mimi sipendi kulizungumzia hilo, kwa sababu tunaona hata Ulaya makosa kama hayo yanafanyika, mchezaji anarudisha pasi fupi, inanaswa watu wanafunga. Au mtu kutolewa kwa kadi nyekundu, inatokea ni mambo ya kimichezo, lakini mimi sitapenda kulizungumzia hilo, tunamuachia mwalimu,”amesema.
  Lakini Aveva amesema Kessy ni mchezaji muhimu ndani ya Simba, ambaye watahakikisha wanampa Mkataba mpya muda si mrefu.
  Jumamosi ya Februari 20, mwaka huu Kessy alimrudishia pasi fupi kipa Muivory Coast wa Simba kipindi cha kwanza ambayo ilinaswa na mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma akaifungia bao la kwanza Yanga katika ushindi wa 2-0, bao lingine likifungwa na Mrundi, AMissi Tambwe kipindi cha pili.
  Na baada ya kosa hilo, mashabiki wa Simba SC wameonekana kupoteza furaha yao kwa Kessy, jambo ambalo lilitarajiwa kuupa wakati mgumu uongozi wa klabu kuamua kumuingezea Mkataba wakati huu wa sasa unamalizika Mei mwaka huu.
  Lakini jana Aveva ametaja maamuzi magumu ya uongozi, kumuongezea Mkataba beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, ambaye anazitamanisha hata Azam FC na mahasimu, Yanga.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAANZA MAZUNGUMZO YA MKATABA MPYA NA KESSY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top