• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 22, 2016

  ZICO: MESSI ATAWAPOTEZA MARADONA NA PELE SASA HIVI, ILA BALLON D'OR MWAKANI YA NEYMAR

  GWIJI wa Brazil, Zico amesema kwamba Lionel Messi anaelekea kuwa Mwanasoka Bora Zaidi wa muda wote, wakati Arsenal inajiandaa kumenyana na timu ya nyota huyo, Barcelona.
  Messi na washirika wake watateremka Uwanja wa Emirates kesho kumenyana na Washika Bunduki wa London katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku washambuliaji pacha wake Luis Suarez na Neymar pia wakitarajiwa kucheza.
  Lakini kiungo wa zamani wa Brazil, Zico anamchukukulia Messi kama mchezaji mwenye kila kitu ambaye hajawahi kutokea.

  Lionel Messi aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 300 katika Ligi Kuu ya Hispania, maarufu kama La Liga baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Sporting Gijon wiki iliyopita PICHA ZAIDI GONGA HAPA

  "Anaanza kuwapiku wachezaji wa kiwango cha Pele, Garrincha, (Johan) Cruyff, (Franz) Beckenbauer na (Diego) Maradona," amesema Zico akizungumza na Barca TV.
  Muargentina Messi hivi karibuni aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 300 katika Ligi Kuu ya Hispania, maarufu kama La Liga na akiwa na umri wa miaka 28 bado ana muda mrefu wa kuendelea kucheza.
  Amewahi kuwafanya vibaya Arsenal miaka ya nyuma, na kinachokumbukwa zaidi ni kuifunga timu ya Arsene Wenger mabao manne peke yake Uwanja Nou Camp mwaka 2010.
  Huku ushirikiano wake na Suarez na Neymar ukizidi kuimarika, Zico anahofia Arsenal itafungwa mechi zote mbili.
  "Utatu wao ni babu kubwa, kwa sababu wanacheza kama timu na kushirikiana vizuri baina yao," amesema Zico, kwa mujibu wa tovuti ya Barcelona.
  "Barca ina nafasi nzuri ya kushinda mechi zote London na Camp Nou."
  Licha ya 'kumzimikia' Messi, Zico amesema kwamba tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, maarufu kama Ballon d'Or ya FIFA mwakani inaweza kuchukuliwa na mchezaji mwenzake wa Barca.
  "Haitakuwa ajabu kabisa iwapo Neymar atateuliwa Mwanasoka Bora wa Dunia,"amesema Zico.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ZICO: MESSI ATAWAPOTEZA MARADONA NA PELE SASA HIVI, ILA BALLON D'OR MWAKANI YA NEYMAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top