• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 21, 2016

  HALL 'AMPIGIA SALUTI' MESSI, ASEMA NDIYE NYOTA WA MCHEZO JANA AZAM IKIUA 3-0 MBEYA CITY

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA
  KOCHA Muingereza wa Azam FC, Stewart John Hall amefurahishwa na kiwango cha kiungo Ramadhani Singano 'Messi' katika ushindi wa 3-0 jana dhidi ya wenyeji Mbeya City kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Hall amesema; "Messi alikuwa mzuri sana katikati na ndiye mchezaji wetu bora katika kipindi cha pili, tulicheza sana mipira mirefu kipindi cha kwanza na kukosa mtu wa kuwaunganisha wachezaji, alipoingia Messi katikati, aliweza kutekeleza vizuri jambo hilo ,".
  Hall amesema kwamba kwa ujumla jana timu yake ilionyesha kiwango safi baada ya kufanyia kazi udhaifu uliojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union kwa kushindwa kuutendea haki mfumo wa 3-5-2 wanaoutumia.
  Ramadhani Singano 'Messi' kulia ameanza kung'ara Azam FC kiasi cha kumkosha kocha Stewart John Hall

  “Tulijitahidi kufanya mazoezi kuondoa kiwango cha chini haraka iwezekanavyo katika mfumo wetu na nadhani leo kiwango chetu kilikuwa cha hali ya juu. Tulianza kwa hali ya chini, tulionekana hali yetu ya kujiamini ilikuwa chini dakika 10 hadi 15 za kipindi cha kwanza na hii ilitokana na matokeo tuliyopata wiki iliyopita (Coastal Union).
  “Lakini baada ya hapo tulianza kujenga vema kiwango chetu na nadhani kipindi cha pili tulikuwa vizuri zaidi, tulifanya mabadiliko ya kimbinu kipindi cha pili, tulimpeleka Messi (Ramadhan Singano) katikati na kumchezesha Farid (Mussa) upande wa kushoto aliyeingia kuchukua nafasi ya Mudathir Yahya,” alisema.
  Hall alisema walifanya mabadiliko ya kumtoa Mudathir ili kuiongezea ubora timu eneo la katikati baada ya kipindi cha kwanza kukosa mtu wa kuwaunganisha vema wachezaji na kubakia kucheza sana mipira mirefu.
  Mwingereza huyo aliongeza kuwa siku zote hawaamini waamuzi na ndio jambo kubwa lililomfanya ampumzishe takribani dakika 25 za mwisho Nahodha Msaidizi Himid Mao na kuingia Frank Domayo, ikiwa ni baada ya kiungo huyo bora mkabaji kuonyeshwa kadi ya njano kipindi cha kwanza.
  Kocha huyo wa zamani wa Academy ya Birmingham City, Zanzibar Heroes na Sofapaka ya Kenya, alisema wanataka kuendeleza ushindi walioupata jana kwa kuifunga Tanzania Prisons licha ya kukiri kuwa itakuwa ni mechi ngumu.
  “Itakuwa mechi ngumu, na siku zote ni ngumu, unajua mechi ya nje siku zote ni ngumu, hivyo tunatakiwa kuendeleza ushindi, lakini kushinda 3-0 ugenini ni matokeo mazuri sana, tunatakiwa kubakia katika hali hiyo ya kujiamini hadi kwenye mchezo ujao,” alimalizia.  
  Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, inatarajia kushuka tena dimbani Jumatano ijayo (Februari 24) kucheza na Tanzania Prisons katika mchezo wa kiporo, ambao unaweza kuipeleka kileleni kwenye msimamo endapo itawachapa maafande hao kwani watafikisha pointi 48 na kuzizidi kete Simba (45) na Yanga (46).
  Matajiri hao wa Azam Complex pia watakuwa wamebakiwa na mchezo mmoja wa kiporo watakaocheza na Stand United Machi 16 mwaka huu.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HALL 'AMPIGIA SALUTI' MESSI, ASEMA NDIYE NYOTA WA MCHEZO JANA AZAM IKIUA 3-0 MBEYA CITY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top