• HABARI MPYA

    Thursday, October 08, 2015

    ULIMWENGU: UCHOVU ULIPUNGUZA MAKALI YETU, WAMALAWI TUTAWAFANYA VIBAYA KWAO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WASHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu na Mbwana Ally Samatta wamesema kwamba walicheza mechi ya jana wakiwa hawako vizuri kwa asilimia 100 kutokana na uchovu.
    Akizungumza kwa niaba ya mwenzake, Ulimwengu alisema kwamba wamepitia mechi ngumu mno wiki iliyopita za Ligi ya Mabingwa Afrika wakimalizia Jumapili na Jumatatu wakaamkia safari ya kuja Dar es Salaam.
    “Tumemaliza mechi na El Merreikh tu, tukaanza mishe (harakati) za safari kuja Dar, kwa kweli tumejituma kutokana na uzalendo wa taifa letu, ili hatukuwa vizuri sana,”amesema.
    Thomas Ulimwengu akifurahia na Mbwana Samatta baada ya kuifungiaTaifa Stars jana

    Samatta na Ulimwengu waliiwezesha Mazembe kukata tiketi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 4-2, ikifungwa 2-1 Khartoum na kushinda 3-0 Lubumbashi.
    Thomas Ulimwengu alifunga bao la ugenini wakati Samatta alifunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0 Lubumbashi na jana wawili hao kila mmoja alifunga bao moja, Tanzania ikiifunga Malawi 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya mchujo wa Kombe la Dunia 2018 Urusi.
    Tanzania itasafiri kesho kwenda Malawi kwa mchezo wa marudiano utakaofanyika Jumapili na mshindi wa jumla atasonga hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ambako atamenyana na Algeria. 
    Kuelekea mchezo wa marudiano, Ulimwengu amesema kwamba anaamini hadi kufika Jumapili watakuwa vizuri na kucheza kwa kiwango cha juu ili kuisaidia Tanzania kusonga mbele.
    “Yaani kwa ujumla tunatarajia kucheza vizuri zaidi kule kwao,”amesema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ULIMWENGU: UCHOVU ULIPUNGUZA MAKALI YETU, WAMALAWI TUTAWAFANYA VIBAYA KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top