• HABARI MPYA

    Friday, October 09, 2015

    TAIFA STARS WAWASILI ‘HOI’ BLANTYRE, MKWASA ASEMA WATAPAMBANA KIUME

    Na Princess Asia, BLANTYRE
    BAADA ya safari ndefu ya kutwa nzima, hatimaye msafara wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ umewasili salama katika mji wa Blantyre, Malawi kuelekea mchezo wa marudiano na wenyeji Jumapili.
    Taifa Stars watakuwa wageni wa The Flames Jumapili jioni Uwanja wa nyasi bandia wa Kamuzu mjini hapa katika mchezo wa marudiano hatua ya kwanza ya mchujo kuwania kupangwa katika makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia 2018 Urusi.
    Wachezaji wamewasili wakiwa wamechoka kutokana na safari ndefu iliyoanza Saa 3:25 mjini Dar es Salaam kwa ndege ya Fast Jet iliyotua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu, Lilongwe Saa 4:05 na timu hiyo ikaenda kupumzuka kwa muda hoteli ya Sun Bird kabla ya kuanza safari Saa 7:05 na kuwasili Blantyre Saa 12 na ushei joni.
    Wachezaji wa Taifa Stars wakati wa kuondoka Dar es Salaam 

    Wenyeji walipanga timu hiyo ifikie katika hoteli ya Victoria, lakini viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania mjini hapa ulikwishaandaa hoteli ya Malawi Sun.
    Hilo lilileta shida kidogo, baada ya askari wa kuongoza msafara wa Stars walipotaka kulazimisha timu iende Victoria, lakini Mkuu wa Msafara, Ahmed Iddi ‘Mgoyi’ akasimama imara kuhakikisha mambo yanakwenda kama yalivyopangwa.
    Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba safari imekuwa ndefu tofauti na walivyofikiria, jambo ambalo limesababisha uchovu kwa wachezaji.
    “Tulitarajia tutatumia saa mbili kwa barabara kutoka Lilongwe hadi Blantyre, matokeo yake tumetumia zaidi ya saa tano. Ni tofauti sana, lakini yamepita. Tunajaribu kutumia muda tulionao kwa maandalizi kaunzia sasa,”amesema.
    Mkwasa amesema usiku huu watafanya mazoezi mepesi katika Uwanja wa jirani na hoteli hiyo, kabla ya kesho asubuhi kufanya pia mazoezi ya kujiweka sawa kuelekea mchezo huo.
    Wachezaji wa Taifa Stars wakiwasili Lilongwe 
     

    Pamoja na kikosi cha Stars kilichofika hapa, lakini kuna msafara wa mashabiki wasiopungua 50 ambao wamekuja kuisapoti timu mjini hapa, wengine kwa ndege na wengine kwa basi.
    Basi la timu ya taifa lilitangulia Blantyire na ndilo lililokuja kuwapokea wachezaji Lilongwe kuwaleta mjini hapa.
    Taifa Stars inahitaji kulazimisha sare Jumapili baada ya Jumatano kushinda 2-0 Dar es Salaam. Na ikifanikiwa kuwang’oa Mwale, itakutana na Algeria katika hatua ya mwisho ya mchujo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS WAWASILI ‘HOI’ BLANTYRE, MKWASA ASEMA WATAPAMBANA KIUME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top