• HABARI MPYA

    Wednesday, October 01, 2014

    KIPA ALIYEZUIWA NA MALINZI KUDAKA JKT RUVU APIMWA KICHWA, YUKO FITI KABISA

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    KIPA wa JKT Ruvu, Jackson Abraham Chove leo amefanyiwa vipimo vya kichwa katika hospitali ya Besta, Kinondoni, Dar es Salaam na kugundulika hana matatizo yoyote, hivyo anaweza kuendelea kucheza.
    Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alimzuia Chove kucheza hadi hapo klabu yake itakapowasilisha vipimo kwamba hana madhara kichwani baada ya kuumia katika mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanania Bara mwishoni mwa wiki.
    Jackson Chove akipimwa leo hospitali ya Besta, Kinondoni, Dar es Salaam

    Chove au Mandanda, alipata dhoruba kichwani katika mechi dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kudaiwa kupoteza fahamu kwa zaidi ya dakika 10, timu hizo zikitoka 0-0.
    Hata hivyo, mwenyewe anasema hakuzimia siku hiyo, bali alipata maumivu yaliyosababisha asikie kizunguzungu hali ambayo baada ya muda ilitulia na akatoka anatembea mwenyewe uwanjani kurejea kambini kwao.
    “Yaani siku ya pili tu mimi niliendelea na mazoezi kama kawaida, tena nikijisikia nipo fiti kabisa, ila imenibidi kutii sheria za wakuu wa nchi na vyeti vitawasilishwa ili niendelee na kazi,”amesema Chove akizungumza na BIN ZUBEIRY jioni hii.
    Baada ya kumkosa Chove katika mchezo wake wa pili wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki, JKT ilichapwa 2-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam langoni akiwa amesimama Benjamin Haule.
    Sasa, kipa huyo anatarajiwa kudaka dhidi ya timu yake ya zamani, Yanga SC Jumapili wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mfululizo wa ligi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPA ALIYEZUIWA NA MALINZI KUDAKA JKT RUVU APIMWA KICHWA, YUKO FITI KABISA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top