• HABARI MPYA

    Wednesday, October 15, 2014

    GRAND MALT YADHAMINI UHURU MARATHON 2014.

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake kisicho na kilevi cha Grand Malt imetangaza kudhamini mashindano ya mbio ndefu za Uhuru ‘Uhuru Marathon’ kwa kiasi cha Sh.  milioni 35.
    Akitangaza udhamini huo jana jijini Dar es Salaam, Meneja wa kinywaji cha Grand Malt, Consolatha Adam, alisema, wameona ni vyema kudhamini mbio hizo kwa sababu zina lengo la kuimarisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
    Alisema huu ni mwaka wa pili kudhamini mbio hizo ambapo mwaka jana kampuni hiyo ilitoa kiasi cha S. milioni 20 na zilifanyika kwa mafanikio.

    Meneja wa kinywaji cha Grand Malt, Consolata Adam akimkabidhi mfano wa hundi ya udhamini wa mbio za Uhuru Marathon 2014, Mratibu wa mbio hizo, Innocent Melleck na kulia.

    Alisema kuwa baada ya kuona malengo yametimia , TBL iliamua kuendelea kudhamini mbio hizo zinazoshirikisha wanariadha kutoka sehemu mbalimbali ndani ya nje ya nchi.
    “Baada ya mwaka jana mbio hizi kufanyika kwa mafanikio makubwa, mwaka huu Kinywaji cha Grand Malt kimeongeza udhamini wake kwa asilimia 75% ambazo ni ongezeko la milioni 15,’’ alisema Adam.
    Ukweli ni kwamba taifa lolote duniani linapigania kuwa na uchumi imara na pasipokuwa na amani hakuna uchumi utakaoweza kukua, hivyo TBL kama kampuni inayotengeza bidhaa za hapa nyumbani imeona ni muhimu kuungana na Watanzania wenzetu wote kuhakikisha kuwa mbio hizi zinafanyika katika hali ya mafanikio makubwa na kuwa za kufana zaidi.
    Aliongeza kwa kuyataka makampuni mengine ya ndani na nje ya nchi kujitokeza na pia kuendelea kutoa chochote walichonacho ili kufanikisha mbio hizi zenye kubeba dhima ya Taifa letu lakini pia wajitokeze kwa wingi kushiriki mbio hizi.
    “Kwa zawadi hizi tulizotangaza leo tunaamini zitakuwa kichocheo kwa wakimbiaji wetu kufanya mazoezi ya kutosha ili kuhakikisha fedha hizi zinabaki ndani ya ardhi ya Tanzania,” alisema.
    Naye mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck, aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo ambazo zina nia kubwa ya kutukumbukusha wajibu wetu wa kutunza na kulinda amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu.
    Alisema zawadi kwa mshindi wa kwanza inatarajiwa kuwa Sh. 2,500,000 kwa wakimbiaji wa kilomita 21 hii ni kwa upande wa wanawake na wanaume.
    Mshindi wa pili kwa mbio hizo iwe kwa upande wa wanawake au wanaume kwa kilomita 21 au ataondoka na Sh 1.500,000 wa tatu Sh 1,000,000 wanne Sh 500,000 watano apata Sh 250,000 na wa sita hadi kumi sh 100,000 kila mmoja.
    Pia mwaka huu kutakuwa na zawadi za ngao za heshima kwa shule za msingi na sekondari zitakazoshiriki mbio za hizo ili kutambua ushiriki wao na tayari shule 25 zimethibitisha kushiriki mbio kwa mwaka huu.
    Mbio hizi zinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam hapo Desemba 7, mwaka huu ambapo zitaanzia na kumalizikia katika Viwanja vya Leaders club.
    Mbio hizi zipo chini ya ulezi wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na kwa mara nyingine tena tunatarajia Mh Rais Jakaya Kikwete kushiriki mbio hizi,
    Mbio hizo zimegawanywa katika makundi makuu matatu ambayo ni kilomita 3 kwa ajili ya viongozi, kilomita 5 kwa watu wote na kilomita 21  ambazo ni maalum kwa wakimbiaji nguli.
    Wadhamini wengine wa mbio hizo ni pamoja na Michuzi Media Group, Jambo Leo, Mwananchi Communication Limited, CXS Africa, Kitwe General Traders, Faza Kidevu Blog, Habari Mseto Blog, Blog ya Wananchi,TBC 1,TBC Taifa,Redio Uhuru.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: GRAND MALT YADHAMINI UHURU MARATHON 2014. Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top