• HABARI MPYA

    Tuesday, July 15, 2014

    SANTOS AWASILI DAR, BHINDA APIGA “YANGA OYEE, MANJI OYEE”

    Na Samira Said, DAR ES SALAAM
    AMETUA. Geilson Santana Santos ‘Jaja’ amewasili Dar es Salaam mchana wa leo, akitokea Brazil tayari kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam. 
    Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC, Mohammed Bhinda ndiye aliyempokea Jaja uwanja wa ndege dar es Salaam kwa mbwembwe kidogo.
    “Yanga oyeee, Manji oyeee,”alisema Bhinda wakati anatoka na Jaja ndani ya Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam (JNIA) mchana wa leo.
    Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC, Mohammed Bhinda kushoto akimpokea Santos JNIA mchana wa leo
    Santos alipokewa na Bhinda JNIA leo
    Jaja na Bhinda wakitoka JNIA tayari kwa safari ya Jangwani


    Jaja anazungumza Kireno tu na hakuweza kuzungumza na Waandishi wa Habari kwa sababu hakukuwa na mkalimani, lakini Bhinda alisema mchezaji huyo ataanza majaribio kesho Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
    BIN ZUBEIRY inafahamu Jaja amekuja Yanga SC kufanya majaribio na kama kocha Mkuu, Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo atamkubali, atafanyiwa vipimo vya afya ambavyo akifaulu pia atasajiliwa.
    Na Yanga SC inataka kumuengua mshambuliaji Mganda, Emmanual Okwi katika usajili wake ili Mbrazil huyo achukue nafasi.
    Yanga inaamua kuachana na Okwi kwa sababu inaamini ni msumbufu na usajili wake uligubikwa na ‘magumashi’ nyingi zilizofanywa na viongozi wa klabu hiyo walioshughulikia suala lake, jambo ambalo limemkera Mwenyekiti Yussuf Manji.
    Yanga SC ina wachezaji watano wa kigeni kwa sasa bila ya Jaja na kabla ya kumtema Okwi, wengine wakiwa ni beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima wote wa Rwanda, Hamisi Kiiza na Coutinho.
    Jaja aliyezaliwa Septemba 21 mwaka 1985 (Miaka 28) mjini Aracaju, Brazil anatokea klabu ya Itabaiana aliyojiunga nayo mwaka 2006 na kabla ya hapo alichezea klabu za Coritiba, Catuense, Olimpico, zote mwaka 2013, Maruinense, Lagarto mwaka 2012, Olimpico tena 2011, Domingos 2010, Confianca 2008 na Sergipe 2007.
    Mbali na Maximo na Coutinho, kocha Msaidizi wa Yanga SC, Leonardo Neiva pia ni Mbrazil ambao wote wanaingia msimu huu.
    Maximo si mgeni Tanzania, kwani kati ya mwaka 2006 na 2010 alikuwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars kabla ya kujiuzulu na kurejea kwao, nafasi yake ikichukuliwa na Mdenmark, Jan Poulsen aliyempisha nduguye, Kim Poulsen ambaye naye ameondolewa na kuajiriwa Mholanzi, Mart Nooij.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SANTOS AWASILI DAR, BHINDA APIGA “YANGA OYEE, MANJI OYEE” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top