• HABARI MPYA

    Monday, April 14, 2014

    KATIBU MKUU WA FIFA AJA DAR

    Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
    KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA), Mfaransa Jerome Valcke atawasili nchini Mei 1, mwaka huu ambapo atafungua semina ya mawasiliano itakayoshirikisha viongozi wa vyama wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
    Akizungumza Dar es Salaam leo (Aprili 14 mwaka huu), Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema Valcke ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuja Tanzania atafuatana na maofisa wengine wa saba wa FIFA.
    Amesema semina hiyo iliyoandaliwa na FIFA itafanyika kwa siku mbili (Mei 1 na 2 mwaka huu) ambapo vilevile Valcke atapata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa.
    Anakuja; Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke atakua Dar es Salaam mwezi ujao

    Rais Malinzi amesema washiriki wa semina hiyo ni marais, makatibu wakuu na wakuu wa mawasiliano wa wanachama 12 wa CECAFA ambao ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somali, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.
    Naye Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga ambaye alifuatana na Katibu Mkuu wake Nicholas Musonye amemshukuru Rais wa TFF kwa kukubali kuwa mwenyeji wa semina hiyo kwani itasaidia katika maendeleo ya mpira wa miguu katika ukanda huu.
    Wakati huo huo: TFF imesema imepokea kwa masikitiko kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Soka (FRAT) Mkoa wa Singida, Josephat Magazi kilichotokea jana mkoani Kilimanjaro.
    Magazi ambaye pia aliwahi kuwa mwamuzi na kamishna wa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) alikuwa amelazwa katika Hospitali ya KCMC. Mazishi yatafanyika kesho (Aprili 15 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwao Ushirombo mkoani Shinyanga.
    TFF imezema msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Magazi alishirikiana na TFF na wadau wengine wa mpira wa miguu katika masuala ya uamuzi na uongozi, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
     Na inatoa pole kwa familia ya marehemu Magazi, FRAT Singida, SHIREFA na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KATIBU MKUU WA FIFA AJA DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top