• HABARI MPYA

    Wednesday, February 05, 2014

    UBALOZI WAWAIBIA SIRI YANGA SC; “AL AHLY WANAKUJA KUWATAZAMA JUMAMOSI”

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    UBALOZI wa Tanzania nchini Misri umewaibia siri Yanga SC kwamba mabingwa wa Afrika, Al Ahly watakuja Dar es Salaam kutazama mechi ya mabingwa hao wa Bara dhidi ya Komorozine ya Comoro. 
    Yanga SC, watafungua dimba nyumbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi na Komorozine ya Comoro katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Kiongozi mmoja wa Yanga SC, ambaye hakupenda kutajwa jina lake ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, wameambiwa na Ubalozi wa Tanzania Misri kwamba kocha mmoja Msaidizi wa Ahly anakuja Tanzania.

    “Wametuambia Ahly wamemuombea viza kocha huyo Ubalozi wa Tanzania kule Misri ili aje kuona mechi yetu na Komorozine. Hatuna shida naye, acha aje, lakini siku hiyo hatutaruhusu watu kuingia na kamera za video kurekodi mechi yetu,”alisema kiongozi huyo wa Yanga. 
    Kwa nini Ahly wanakuja kuipiga chabo Yanga SC? Ni kwamba iwapo mabingwa hao wa Bara watafanikiwa kuitoa Komorozine baada ya mechi mbili za nyumbani na ugenini ndani ya wiki mbili, watakutana na Al Ahly katika Raundi ya Kwanza.   
    Yanga SC ipo kambini Bagamoyo mkoani Pwani ikijiandaa na mchezo huo wa Jumamosi ambao wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri. 
    Wakati Yanga ikianza na Wacomoro, Azam FC nao wataanzia nyumbani pia na Ferroviario Da Beira ya Msumbiji katika Raundi ya Awali ya Kombe la Shirikisho wikiendi hii.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UBALOZI WAWAIBIA SIRI YANGA SC; “AL AHLY WANAKUJA KUWATAZAMA JUMAMOSI” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top