• HABARI MPYA

    Wednesday, February 05, 2014

    SHIBOLI AINGIA MITINI, KMKM NA CHUONI ZAENDA VITANI AFRIKA

    Na Salum Vuai, Zanzibar
    KATIKA hali ya kustaajabisha, mshambuliaji wa KMKM Ali Ahmed Shiboli, ameingia mitini saa chache kabla timu yake hiyo kupanda ndege kwa safari ya Addis Ababa nchini Ethiopia, kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Dedebit FC.
    Habari zilizopatikana kutoka katika uongozi wa washika magendo hao wakati msafara wao ukiwa uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume Zanzibar leo mchana, zimeeleza kuwa, mapema asubuhi ya leo, mchezaji huyo alibeba mkoba wake wa safari na kuwaaga wachezaji wenzake kwamba anakwenda mjini kidogo na baadae atarejea kambini.
    Ally Ahmed Shiboli ametoweka

    Lakini hadi mabaharia hao wanakwea pipa kwenda Ethiopia, mshambuliaji huyo alikuwa hajarejea.
    Hata hivyo, pasi yake ya kusafiria imo mikononi mwa viongozi wa timu pamoja na za wachezaji wengine, na tiketi yake imebaki katika kaunta za uwanja wa ndege.
    Viongozi wa timu wameelezea kusikitishwa na kitendo cha Shiboli, na kusema kuwa watakaporejea nchini watawasilisha malalamiko dhidi yake katika Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kwa hatua zaidi.
    Baada ya kukimbia kwa Shiboli ambaye simu yake haipatikani tangu wakati huo, wachezaji walioondoka ni makipa Mudathir Khamis na Salum Amour, pamoja na Pandu Haji, Faki Hamad, Kassim Abdulkadir Nemshi, Khamis Ali, Haitham Khamis, Iddi Kambi, Ibrahim Khamis, Vent Kamanya, Nassor Ali, Juma Kizungu, Mudrik Muhib, Maulid Kapenta, Ame Khamis na Haji Simba.
    Viongozi ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya ZFA Hashim Salum, Mohammed Sheha (Katibu), Khatib Khamis (Mwenyekiti), Hassan Ameir (Daktari), Ali Bushir (Kocha mkuu) na msaidizi kocha Ali Shein.
    KMKM itashuka dimbani Jumapili alasiri kumenyana na Dedebit FC.
    Nayo timu ya Chuoni inayopeperusha bendera ya Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, inatarajiwa kuondoka uwanja wa ndege wa Zanzibar mnamo saa 9:00 usiku wa kuamkia kesho Alkhamisi Febuari 6 kwenda Harare Zimbabwe.
    Timu hiyo imepangwa kuanza resi za kuwania taji hilo dhidi ya klabu ya Howmine, siku ya Jumamosi mnamo saa 9:00 majira ya Zimbabwe.
    Msafara wa Chuoni unajumuisha wachezaji 18 ambao ni Yussuf  Mohammed, Ahmed Ali, Ramadhan Hamad, Mwinyi Haji, Ahmed Mohammed, Abdulrahman,  Saleh Hamad, na Adam Hamad, Ahmed Abbas, Moka Shaaban, Hamad Mshamata, Ibrahim Rajab, Ame Ali, George Thomas, Bakari Ayoub, Amour Bakari, Abdulkadir Ibrahim na Hussein Rashid.
    Viongozi ni Rais wa timu Maalim Juma ambaye anaongoza msafara huo, Simai Uzia (Kaimu Mwenyekiti), Juma Salum (Mjumbe wa ZFA), Ali Abdalla (Kocha mkuu) Ali Bakari Mngazija (Msaidizi kocha) na daktari wa timu Ahmed Mgeni.
    Makocha wote wawili, Ali Bushiri wa KMKM na Ali Abdallah wa Chuoni, wameelezea matumaini yao ya kufanya vyema katika michezo ya hiyo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye hatua ya pili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHIBOLI AINGIA MITINI, KMKM NA CHUONI ZAENDA VITANI AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top