• HABARI MPYA

    Tuesday, February 11, 2014

    KALI ONGALA AACHWA AZAM FC SAFARI YA MSUMBIJI, KIKOSI CHAONDOKA KESHO KUPITIA AFRIKA KUSINI

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Kalimangonga Sam Daniel Ongala ‘Kali Ongala’ hatakuwamo kwenye msafara wa timu hiyo unaokwenda Msumbiji kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali Kombe la Shrikisho Afrika dhidi ya wenyeji Ferroviario de Beira mwishoni mwa wiki.
    Menaja wa Azam FC, Jemadari Said ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, Kali raia wa Uingereza mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliyekulia Sinza mjini Dar es Salaam, atakosa safari hiyo kwa sababu pasipoti yake imeisha.
    Pasipoti imemkwamisha; Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala kushoto akiwa na bosi wake Joseph Marius Omog

    Hata hivyo, Jemedari hakusema kama mtoto huyo wa mwanamuziki maarufu wa zamani nchini marehemu Dk Remmy Ongala kama ataungana na timu hiyo Msumbiji atakapomaliza matatizo ya pasipoti yake au la. 
    Azam FC iliyoanza kwa ushindi mwembamba wa 1-0 Jumapili Uwanja wa Azam Complex Jumapili, itaondoka kesho Saa 4:00 asubuhi kwa ndege ya Fast Jet hadi Johannesburg, Afrika Kusini ambako wataunganisha ndege ya shirika la Msumbiji kwenda Beira itakapochezwa mechi hiyo.
    Azam itaondoka na wachezaji 21 ambao ni makipa; Mwadini Ali, Aishi Manula na Jackson Wandwi, mabeki Luckson Kakolaki, Erasto Nyoni, Malika Ndeule, Aggrey Morris, Said Mourad, David Mwantika, viungo Ibrahim Mwaipopo, Kipre Balou, Jabir Aziz, Salum Abubakar, Himid Mao, Khamis Mcha na washambuliaji John Bocco, Kipre Tchetche, Brian Umony, Seif Abdallah, Gaudence Mwaikimba na Ismael Kone.
    Benchi la Ufundi litaongozwa na Kocha Mkuu Mcameroon, Joseph Marius Omog, kocha wa makipa Iddi Abubakar, Meneja Jemadari Said, Daktari Mkuu Mwanandi Mwankemwa, Mchua misuli Paul Gomez na mtunza vifaa Yussuf Nzawila. 
    Azam inahitaji sare yoyote baada ya ushindi wa 1-0 nyumbani ili kusonga mbele.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KALI ONGALA AACHWA AZAM FC SAFARI YA MSUMBIJI, KIKOSI CHAONDOKA KESHO KUPITIA AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top